Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Novemba 21, 2020

Jumamosi, Novemba 21, 2020,
Juma la 33 la Mwaka wa Kanisa

Kumbukumbu ya kutolewa Bikira Maria Hekaluni

Zek 2:14-17;
Lk 1:46-55;
Mt 12:46-50

SADAKA ILIYO KAMILI!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha sikukuu ya kutolewa Bikira Maria hekaluni. Ni siku inayoonesha kwamba Bikira Maria alikuwa chombo kiteule cha Mungu, kilichoandaliwa na Mungu tangu kuzaliwa kwake na wazazi wake walikuwa wacha Mungu waliomuandaa vizuri kiroho.

Kwa desturi za kabila la Israeli na kuendana na sheria ya Mungu, sheria ilikuwa ya kuwatolea watoto hekaluni iliwahusu wanaume walio vifungua mimba tu-wanawake hawakulazimika kisheria. Kitendo cha Maria kutolewa hekaluni chaonesha kwamba wazazi wake walifanya mpaka ziada, walifanya zaidi ya kile cha sheria na hii kwa kweli ilionesha umuhimu wa Bikira Maria kama chombo kiteule cha Mungu. Hii ndiyo kumbukumbu yetu ya leo ilivyo na masomo yetu ya leo yanatusaidia vizuri kutafakari kumbukumbu hii.

Somo la kwanza kutoka katika kitabu cha nabii Zekaria. Hapa tunaona Mungu akionesha kupitia kwa nabii Zekaria kwamba Israeli ni chombo kiteule cha Mungu kilichochaguliwa na Mungu kwa kazi yake maalumu. Hivyo anaahidi kuwatetea, kupambana na mataifa yaliyowatesa na lengo la kufanya hivi ni kumfanya Israeli awe mfano kwa mataifa mengine-yaani mataifa mengine yakitaka kumjua Mungu wa kweli waende Israeli, wakitaka kuona litrujia safi waende Israeli, wakitaka kuona uongozi mzuri waende Israeli; hivyo, lengo lilikuwa ni wote waone, waache uovu na wamgeukie Mungu wa kweli.

Hapa tunaona kwamba japokuwa Israeli alikuwa chombo kiteule cha Mungu, alikuwa na wajibu wa kutimiza pia; alipaswa kuhakikisha anashika sheria ya Mungu na kuepuka kuwakwaza wengine, ili awe mfano kwa wengine katika kumjua Mungu.

Yesu anapigilia msumari suala hili kwa kusema kwamba heri yule anayelisikia neno la Mungu na kulishika; huyo ana heri kwani kwa maisha yake atawaongoza wengi kwa Mungu; atamfanya Mungu atukuzwe na wengi.

Kinachosemwa katika haya masomo ndicho kilichotokea kwa Maria. Yeye alikuwa chombo kiteule cha Mungu na kwa sababu hiyo aliamua kutokumwangusha Mungu. Alihakikisha anaishika kweli sheria ya Mungu na ndio sababu za kutolewa hekaluni lengo ni kuishi sheria ya Mungu.

Ndugu zangu, kwa utii wa huyu Mama, dunia ilipata ukombozi, dunia iliokolewa kutoka katika dhambi ya asili na sasa tuna mkombozi wetu Yesu Kristo. Shukrani sana kwa utii wa Bikira Maria, shukrani sana kwa wazazi wake.

Ndugu zangu, kwetu sisi, Wakristo sherehe hiii ina ujumbe mzito kwetu. Kwa ubatizo wetu nasi tumetolewa hekaluni. Tunapaswa kutambua hili. Hivyo, ishi kanuni za Kristo. Jua kwamba ukiishi ukristo wako vyema, unawafanya wengi wamtukuze Mungu, unakuwa chanzo cha wengi kuja kwa Mungu, unasaidia utawala wa Kristo uendelee Zaidi. Lakini ukiishi bila kufuata mashauri ya Kristo, unamsaidia shetani kuendeleza mamlaka yake, unakuwa mjumbe, balozi wake, yaani unamdidimiza Kristo na shetani anaanza kutawala.

Hivyo, muonee Kristo huruma jamani. Ameshakuja na kufa hapa duniani. Mateso yote yale aliyompata na bado unazidi kumtumia shetani kama mvuvio wako? Niambie shetani alishawahi kumwaga hata tone moja la damu yake ili akuokoe? Niambie ndugu yangu. Hivyo, jua kwamba ukikataa kuishi maisha ya Kikristo vizuri, ukiwa unaendelea kutenda dhambi, ukiwa unatazama mapicha mapicha kwenye simu yako tena ya ajabu ajabu-jua kwamba unasaidia utawala wa shetani kukua.

Hivyo, siku ya leo tutafakari sheria zetu na tuziishi, tusimwachie mwanya shetani.

Maoni


Ingia utoe maoni