Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Novemba 13, 2020

Ijumaa, Novemba 13, 2020,
Juma la 32 la Mwaka wa Kanisa

2Yn 1:4-9
Zab 118:1-2, 10-11, 17-18
Lk 17:26-37

KUJIWEKA TAYARI KWA UPENDO!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu inaongozwa na zaburi yetu ya wimbo wa katikati inayosisitizia kwamba wana heri wale waitiio sheria ya Bwana. Umuhimu wa sheria hii ni kumfundisha mtu hekima. Na kweli utashangaa, wale wanaokazana kuitambua sheria ya Bwana huishia kuwa na moyo wa hekima mara nyingi hata zaidi ya wale walio hata na kisomo kikubwa.

Utashangaa kuona maandishi ya baadhi ya watakatifu ambao waliyaandika katika sala. Mafundisho yao huvutia zaidi kuliko yale ya wenye elimu ya kidunia. Hata wahubiri wanaosali kabla ya kuhubiri huishia kutoa mahubiri mazuri zaidi. Kweli sheria ya Bwana humfunza mjinga hekima na kumtii Bwana ni chanzo cha hekima hii. Tumtii Bwana nasi tutapata hekima. Ndio maana utashangaa kuona kwamba wengi wanapendelea kesi zao ziamuliwe na viongozi wao wa dini kuliko na mahakimu waliopo mitaani. Sheria ya Bwana humfundisha mtu hekima.

Huu ujumbe wa zaburi unasisitizia vyema ujumbe wa Yohane katika somo la kwanza kwamba ni wale tu wanao yatii mafundisho ya Bwana wanaweza kuwa na Roho wa Bwana. Manabii wa uongo wanakosa utii ndio maana wanamkosa Roho wa Bwana. Sisi tuwe watii na wanyenyekevu zaidi, tuikumbatie sheria ya Bwana na hakika tutakuwa na hekima zaidi. Maisha yetu yamekosa mvuto kwa wengi kwa sababu ya ukosefu wa utii kwa Bwana. Tuzidishe uchaji kwa Bwana nasi tutakuwa na hekima na mvuto kama wana wa Mungu.

Yesu katika Injili anasema siku za mwisho wana wa dunia hii bado watakuwa wanaonesha mizaha mizaha tu na kutokujiandaa kama walivyomfanyia Nuhu. Aliijenga safina kwa miaka 120 lakini hakuna aliyebadilika hadi ile siku ya gharika na watu kuangamia.

Sisi tuache mizaha kwa mambo ya Mungu. Mambo ya Mungu tunayafanyia mno maigizo. Wengine tunayatumia kufichia uovu wetu. Kama tumeamua kubadilika tuanze kweli. Mizaha na ukosefu wa maamuzi sahihi yanatuangusha kwa kiasi kikubwa sana. Na Yesu amedhihirisha kwamba kutakuwa na uchaguzi-mnaweza kuwa wawili mahali pamoja lakini mmoja atatwaliwa na mwingine aachwa. Wale wenye mizaha mizaha ndio watakao achwa na wengine kutwaliwa. Tuache mizaha hii ndugu zangu. na tusiyaone mambo matakatifu kama maigizo. Tuache kufanya maigizo na mambo matakatifu. Wengi tumezidisha maigizo na mambo haya. Tusiyatumie kufichia uovu wetu.

Maoni


Ingia utoe maoni