Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Novemba 14, 2020

Jumamosi, Novemba 14, 2020,
Juma la 32 la Mwaka wa Kanisa


3Yn 1:5-8;
Zab 111:1-6;
Lk 18:1-8

KUVUMMILIA KATIKA SALA!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu inaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na Yohane akiwahimiza waamini kuwapokea wamisionari na viongozi wao wa dini. Wasiwaache wahangaike au kunyanyaswa na wapagani bali wawe baba na mma kwao.

Ilikuwa rahisi kwa wamisionari kunyanyaswa kwa sababu waliishi mbali na nyumbani na kwa kiasi kikubwa walitegemea misaada. Hivyo kama watakutana na Wakristo wasiowakarimu, moja kwa moja waliishia hata kuangukia mikononi mwa wapagani ambao waliwanyanyasa. Wakristo wa mwanzo waliwajali sana wamisionari wao kuepuka wasinyanyaswe na wapagani.

Hili nasi tuliige leo.Tusiwatupe wamisionari wetu, mapadre, masista, makatekista-tusiwatupe. Hawa hufanya kazi mbali na nyumbani mwao. Tunapaswa kuwa baba na mama kwao. Tukiwaacha watanyanyaswa na wapagani, watakwenda kufanya biashara huko na wapagani watawanyanyasa hata kuwafunga gerezani. Tusikubali hili. Tusikubali waangukie mikononi mwa wapagani-tusikubali wanyanyaswe na wapagani. Tuwatunze kama kaka na wadogo zetu, wajisikie nyumbani kabisa. Tusikubali ardhi wanayoitunza kwa ajili ya kanisa inyanganywe toka kwao hivihivi na watu wapagani. Tuwatee. Tusikubali kabisa waonewe. Tuwalishe wamisionari wetu kwa kuwa wakarimu kwao ili waendeleze kazi ya Kristo vyema.

Katika injili, Yesu anahimiza tusikate tamaa, tuombe bila kuchoka, kuomba inahitaji unyenyekevu, ni wale tu wenye unyenyekevu wanaofanikiwa. Wengi wetu tunashindwa kuomba kwa sababu ya kutokujishusha na tunataka tupate haraka.

Tusije na roho ya namna hii mbele ya Mungu kila tuendapo kwa maombi mbele ya Mungu. Mungu anahuruma kubwa kuliko huyu kadhi. Kama kadhi aliweza kumpatia huyu mama haki yake, hakika Mungu atatupatia na sisi haki zetu tena kwa ziada kubwa kabisa. Nasi tuwe tayari kuwapatia wenzetu haki zao.

Tusizungushezungushe watu. Tuwapatie iliyohaki yao na wajapo kwetu mara kwa mara, tusionyeshe ugumu wa moyo-tufungue mioyo yetu na kuwapatia haki yao. Tusikubali kuwa sababu ya kilio kwa wengine. Wapo waliodhulumiwa ardhi, nyumba na mali mbali mbali ambao daima hutokwa na machozi, hakika Mungu atawasikia na anayedhulumu hatabaki salama kwani huwezi kupigana na Mungu.

Maoni


Ingia utoe maoni