Jumatano, Novemba 11, 2020
Jumatano, Novemba 11, 2020.
Juma la 32 la Mwaka
Tit 3:1-7;
Zab 23
Lk 17: 11-19.
SHUKRANI!
Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo katika adhimisho la Misa Takatifu. Leo katika zaburi yetu ya wimbo wa katikati, tunakutana na Daudi akitoa ushuhuda wa jinsi Mungu alivyomchungaji mwema kwa wale wanaomba ulinzi kwake. Yeye mwenyewe aliomba ulinzi huu na kuupata kwa kuwa maisha yake yalijawa na misukosuko ya kutafutwa auawe.
Ndivyo ilivyo hata kwa nyakati zetu. Labda baadhi yetu tunaishi katika ujirani mgumu kiasi kwamba wanaokuzunguka wanataka hata nafsi yako iangamie lakini ni kwa sababu tu hawana uwezo wa kufanya hivyo. Hata ukiwa na hakika na ukweli kuna baadhi ya watakaokuchukia. Katika mazingira ya namna hii hatuna jinsi isipokuwa kujikabidhi mikononi mwa Mungu na kuomba ulinzi kama alivyofanya Daudi. Na silaha kuu itakayotuokoa hasa katika lile eneo tunapochukiwa na wenzetu ni kuishi maisha mema yasiyo na 'scandals', dhambi au kulipiza kisasi. Maisha mema ndiyo yatakayotufanya tuwashinde maadui wa namna hii.
Ndiyo Paulo anayomsisitizia Tito kuyasisitizia katika somo la kwanza. Kipindi hiki wakristo walikumbwa na maadui wengi na kilichowaokoa ni sala na maadili yao mema. Sisi tutambue kwamba maisha mema yasiyolipiza kisasi ni silaha ya kumshinda adui. Mara nyingi tunashindwa na maadui kwa sababu wanatukamatia kirahisi katika uovu au 'scandals' zetu na hapa wanatufunga mdomo. Tuishi maisha mema iwe silaha yetu katika Bwana.
Kwenye somo la injili Yesu anafurahishwa na kitendo cha mkoma Msamaria kuja na kutoa shukrani. Wasamaria hawakuelewana vizuri na Wayahudi. Yesu kama Myahudi anamtendea wema mkuu bila ya kujali uhusiano wao wa kiasili na hili tendo jema linamfunga mdomo huyu Msamaria na anadiriki kuja na kujitupa miguuni mwa Myahudi kushukuru.
Sisi tusiache kuwafanyia 'surprise' maadui zetu kwa kuwatendea mambo mema hata kama wao wanatutendea mabaya au kutuwazia mabaya. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni