Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Novemba 12, 2020

Alhamisi, Novemba 12, 2020,
Juma la 32 la Mwaka wa Kanisa


Flm1:7-20;
Zab 145:7-10;
Lk 17:20-25


UFALME WA MUNGU UPO KATI YETU.

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana linaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati ambapo tunakutana na maneno yasemayo ana heri yule anayesaidiwa na Bwana. Bwana asipokusaidia kusonga mbele itakuwa tabu sana. Tunakuwa kama wale waliokuwa wanajenga mnara wa Babeli-badala ya kujenga walibomoa au wana Wamisri walipokuwa wanawakimbiza waisraeli ndani ya ile bahari-mambo yalienda kinyume chao. Bwana akienda kinyume nasi tutakwama katika mengi-tutalima hatutavuna, tutavuna na kushindwa kula-kama ilivyotokea kwa yule tajiri mpumbavu, na tutakula pasipokuwa na afya kama inavyojitokeza kwa baadhi yetu kila siku.

Wengi tumevuna mali tukashindwa hata kuila, na wale tunaoila hata hatupati afya-ni matatizo kila siku. Mambo kama haya yanatukumbusha tumrudie Mungu na kumtegemea zaidi.

Katika somo la kwanza, Honesmo ndiye anayeonyesha kusaidiwa na Bwana. Yeye kabla ya kujiunga na ukristo, alikuwa mtumwa aliyemilikiwa na mwingine lakini baada ya kuingia ukristo-ukristo unamrudishia utu wake na Paulo anachukua muda kumwelezea Bwana wa huyu Honesmo kwamba ampokee kama mtoto wake kama ambavyo angempokea yeye. Huu ndio ukuu wa imani yetu kwa Kristo. Kwa kweli ni ya thamani kubwa. Tuitunze vyema imani hii.

Na pia tuwaone wenzetu hata kama ni maskini kuwa watu wenye hadhi. Kwa njia ya imani yao katika Kristo, wamepewa utu. Tutumie utu huu vyema. Tusinyanyase yeyote.

Somo la injili linazungumzia juu ya ujio wa ufalme wa Mungu. Anasisitizia kwamba ufalme wa mbinguni upo katikati yao. Hapa alimaanisha zaidi kwamba ufalme huu unapaswa uwe moyoni mwao.

Mioyo yetu iutangaze ufalme huu kwa kile kinachotoka ndani yake, kwa maneno tunayosema na kinywa chetu, mawazo yetu na matendo. Wengi bado tunatangaza ufalme wa shetani kutokana na picha tunazotuma, miziki tunayosikiliza, filamu tunazoangalia na muda tunaotumia katika kuangalia picha mbaya ndani ya simu zetu. Vitu vya Mungu hatuvipatii muda, hata ile siku ya Jumapili bado inaonekana kama siku ya starehe na anasa kuliko kusali. Dhambi nyingi zinatendeka ndani ya siku hii ya jumapili kuliko siku nyingine. Tuombe kutangaza utawala huu kwa umakini zaidi.

Maoni


Ingia utoe maoni