Jumanne, Novemba 10, 2020
Jumanne, Novemba 10, 2020,
Juma la 32 la Mwaka wa Kanisa
Tit 2:1-8, 11-14;
Zab 36:3-4, 18, 23, 27, 29;
Lk 17:7-10
MTUMISHI MWAMINIFU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo katika zaburi yetu ya wimbo wa katikati tunakutana na maneno kwamba Bwana huwapatia wokovu wote wamchao. Hivyo zaburi hii inawatia moyo wale wamtumainiao Bwana waendelee kumtegemea na wale wasiomtegemea Bwana wazidishe bidii. Ni mwaliko kwamba kila mmoja wetu awekeze kwa Bwana kwani Bwana haachi kumpatia wokovu yeyote awekezaye kwake.
Zaburi hii inatumika kutilia mkazo ujumbe wa Paulo kwa mfuasi wake Tito. Kipindi hiki Paulo alijiona kufikia mwisho wa utume wake na hivyo alimtegemea zaidi Tito. Tito alipaswa kuonesha mfano na kuwasisitiza watu kufundisha kwa njia ya mfano wao wa kimaisha. Kina mama wenye umri wanaalikwa kuwa mfano kwa kina mama wadogo; mfano wa utii hasa kwa waume zao. Na kinababa wenye umri wanapaswa kuwa mfano kwa waliowachanga hasa katika suala la tamaa kwamba wasiwe watu wa tamaa.
Somo hili linamgusa kila mmoja wetu kwa siku ya leo. Linatueleza kwamba umri ni lazima uendane na hekima pia. Lakini kuna kati yetu ambao kadiri umri unavyoongezeka, ndivyo hekima yetu inapungua. Hapa yabidi kumuomba Mwenyezi Mungu ili hekima yetu iongezeke. Tunapozeeka bila hekima yetu kuongezeka ni aibu kubwa kwa upande wetu kwani tunaangaliwa na wengi. Tuone uchungu tunapokutwa tukipigana vikumbo au kubishana pengine na wajukuu wetu tukigombania vitu vya kijinga tu. Tuombe Mungu atufanye hekima yetu iongezeke kadiri ya umri wetu pia.
Injili ya leo inatufundisha tunganganie utumishi. Utumishi ni hekima tosha ambayo inatupasa ikue pamoja nasi kadiri umri unavyoongezeka. Hii inatusaidia kuishi na wengi ndani ya dunia hii na kuepuka makwazo mengi. Mara nyingi sisi tulio na umri tunagombana na wale wadogo kwa sababu mara nyingi tunataka wao watutegemeze na kututumikia. Lakini tutakapogeuza mtazamo ili nasi tuwategemeze-hakika tutaishi nao katika amani kubwa.
Tuombe kuishi utumishi. Hii ndio hekima inayopaswa kukua nasi kadiri ya umri wetu unavyoongezeka maishani. Namna hii tutakuwa mfano.
Maoni
Ingia utoe maoni