Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Novemba 07, 2020

Jumamosi Novemba 7, 2020
Juma la 31 la Mwaka

Flp 4:10 – 19
ZAB. 112:1 – 5 (K) 1
Lk. 16:9-15

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo katika adhimisho la Misa Takatifu. Leo tafakari yetu inaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati inayosisitizia heri kwa yeyote amchaye Mwenyezi Mungu. Huyu atatulia kabisa, na kuwa na moyo thabiti. Hatayumbishwa na vitu kama njaa, ukosefu wa fedha, elimu au cheo. Yeye moyo wake utatulia kwa Bwana.

Moyo wa namna hii ndio aliokuwa nao Paulo katika somo la kwanza. Yeye alimtegemea Mungu na hivyo basi haogopeshwi na misukosuko yote ya ulimwengu huu. Hashtushwi na njaa au kushiba, utajiri au umaskini, kuwa navyo au kutindikiwa. Amekwishajifunza kuvumilia hali zote. Ukiona tunayumbishwa na mambo kama haya, basi tutambue kwamba hatumchi Mungu. Kweli kukubali kukosa usingizi au kupata pressure ati kwa sababu nimekosa Pesa ya kunywa bia au nimekataliwa na msichana au kijana amenikataa-au wenzangu wamependelewa kuliko mimi ni dalili za kutokumcha Mungu.


Mungu hutuwezesha kuyaweza mambo yote. Tunapokubali kushindwa na vidogo hivi ni lazima tujiulize-je?-kweli ninamtegemea na kumcha Mungu, kwa nini nipewe pressure na kitu hiki? Tumtegemee Mungu tupate kuzishinda hali za namna hii.

Katika injili Yesu anasema kwamba hatuwezi kuwatumikia mabwana wawili-mara nyingi ukitumikia mali na Mungu kwa wakati mmoja, kinachotokea ni kumnyima Mungu nafasi. Unaifanya ile mbegu iliyooteshwa isongwe na miiba ya ulimwengu na itashindwa kuzaa. Wengi wetu hata siku ya jumapili hatuendi kanisani ili tufanye biashara. Ukweli ni kwamba ukianza kwa kutumikia mali, utamtupa Mungu pembeni tu na utamkosa. Lakini ukianza kwa kumtumikia Mungu utapata yote.

Tupambane na uchoyo, tumpatie Mungu haki yake, ili basi tupate kubarikiwa naye. Tumtolee sadaka bora kama Abeli. Tuache kumtolea vile vitu vya mwisho au chenchi au zile pesa zilizotoboka na kuchanika. Tumpe Mungu kile kilichobora kukiri ukuu wake.

Maoni


Ingia utoe maoni