Alhamisi, Novemba 05, 2020
Alhamisi, Novemba 5, 2020
Juma la 31 la Mwaka
Flp. 3:3 – 8
Zab. 105:2 – 7 (K) 3
Lk. 15:1-10
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu inaongozwa na maneno ya zaburi yetu ya wimbo wa katikati kwamba enyi mumtafuato Bwana mioyo yenu ifurahi; wajivunie jina na matendo ya Bwana.
Furaha ya namna hii ni dhihirisho la roho iliyotulia, inayoridhika, isiyo na tamaa, imetoshekwa na kile Bwana alichotoa na hivyo basi inakuwa na kila sababu ya kufurahi. Furaha na kuridhika na utulivu ni viashirio vya roho iliyobarikiwa na Bwana.
Paulo katika somo la kwanza anaonesha kuridhika na imani yake na neema Kristo alizomjalia kiasi cha kuwa tayari kutangaza wema huu. Kama asingalikuwa na furaha na kuridhika katika imani yake mpya hakika asingaliweza kuwashawishi Wafilipi wajiunge naye. Nasi lazima tuonyeshe furaha na kuridhika katika imani yetu na Ukristo wetu.
Tuwe na furaha, furaha ni ushuhuda unaowavutia wengine kuja kwa Kristo. Furaha inamvuta mwingine. Sisi tukiwa watu wa huzuni na kulalamika katika maisha huwa tunawakwaza wengine kumfuata na kumwamini Mungu.
Katika injili, Yesu anaeleza kwamba amekuja kuwatafuta waliopotea. Anakiri kwamba mbele ya Mungu wanadamu wote wanahadhi sawa na wanapendwa kabisa. Hata wale wanaokataa upendo huo bado anazidi kuwatafuta ili basi awaokoe na wanapokubali kweli kunakuwa na furaha kubwa sana.
Somo hili limguse kila mmoja wetu leo. Pale tunapoungama na kukataa dhambi ama kweli ni furaha kubwa kwa Yesu. Sisi tunaoishi uasherati, kuishi uchumba sugu-pale tutakapoamua kufunga ndoa na kuacha dhambi hizo ama kweli itakuwa ni furaha kubwa sana mbele ya Mungu. Leo tuache vilema vya dhambi leo. Pia tuwe wavumilivu zaidi katika kuwatafuta waliopotea-unaposhindwa kumrudisha aliyemdhambi kundini na kumwacha aangamie-jua kwamba ni kushindwa mtihani na hapa tunakuwa tumeshindwa vibaya zaidi. Sisi tusiwe watu wa kukata tamaa kwa haraka na tuzidishe bidii katika kuwavuta wenzetu waliopotea.
Maoni
Ingia utoe maoni