Jumatano, Novemba 04, 2020
Jumatano, Novemba 4, 2020.
Juma la 31 la Mwaka
Flp: 2:12-18;
Zab 27: 1.4.13-14,
Lk 14: 25-33.
GHARAMA YA KUWA MFUASI!
Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu katika adhimisho la Misa Takatifu; tafakari yetu ya leo inaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati; na hapa tunamkuta mzaburi akitangaza waziwazi kwamba Bwana ndiye ngome yake na hakika hakuna cha kumtisha. Huu ni ushuhuda aliotoa Daudi kwani maishani mwake aliionja huu ulinzi maalumu wa Bwana na leo anashuhudia mbele yetu kwamba Bwana hakika ndiye alikuwa nguvu na ngome yake.
Ujumbe huu wa Daudi unatilia mkazo pia ujumbe wa Paulo katika somo la kwanza. Paulo anawasisitizia Wafilipi kujenga maisha yao katika Bwana. Wabakie watu wa imani na utii hata kwa kile kipindi ambacho yeye hayupo kwao-wazidi kubakia kuwa wema. Hii itawafanya wangae mbele ya watesi wao, mbele ya ulimwengu uliopotoka.
Ndilo na sisi tunalokumbushwa na Paulo leo. Tumwambie Bwana kwamba wewe ni Mwamba wetu. Hapa tutaweza kungaa ndani ya huu ulimwengu tukiwa nawe. Tukikosa hili kwa hakika ndio tutakuwa tumekosa yote. Sehemu nyingi hatungai, tunakuwa watu wa kuleta giza. Tunapokataa ukweli, kuwa watu wa kusingizia watu, kuiba vya wengine, kuwatetea wenye navyo, na kukataa kuwasaidia majirani zetu hapa tunatoa giza. Haya ni matendo yanayotufanya tushindwe kungaa.
Tufanye matendo yatakayotufanya tungae tukiwa na Bwana.
Kwenye injili yetu leo tunakutana na Yesu akisema kwamba kama hatuko tayari kubeba msalaba kwa hakika hatutaweza kuwa wafuasi wake. Mfuasi wa Yesu lazima uoneshe utayari wa kuvumilia. Hii ni tunu muhimu. Sio tunaogopa na kushindwa kuvumilia hata kwa vitu vidogovidogo tu. Ni aibu kila siku kwa wakristo kushindwa na vitu vidogo vidogo kwa kukosa uvumilivu. Wakristo wa mwanzo walionesha ukomavu kwa kuwa hodari katika kuvumilia na wakafanikiwa sana.
Sisi tusiwe watu wa kuogopa shida, tuvumilie misalaba ya familia zetu, masomo, rafiki na majirani. Kwa uvumilivu wetu, tutayaokoa maisha yetu. Wengi tutapoteza mengi kwa sababu ya kukosa uvumilivu. Tumuombe Mungu atusaidie.
Maoni
Ingia utoe maoni