Jumanne, Novemba 03, 2020
Jumanne, Novemba 3, 2020
Juma la 31 la Mwaka
Flp 2: 5-11;
Zab 22: 25-31;
Lk 14: 15-24.
MAJUKUMU YA KIKRISTO!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Mungu katika zaburi yetu ya katikati, kwenye shairi la kwanza tunakutana na maneno yasemayo kwamba maskini watakula na kushiba. Hawa wanakula si kwa sababu ya kuwa na uwezo au pesa za kuwashibisha bali hali yao ya kinyenyekevu na udogo na utayari wao ndio utakaowafanya washibe.
Dhana ya utayari katika somo la kwanza tunaona ikimfanya Yesu akwezwe juu kuliko vyote-utayari wa kukubali kufa msalabani ambako kwa Wayahudi ilikuwa ni kulaaniwa lakini akawa tayari kuchukua laana na kweli akapata ukuu.
Wale wanaoalikwa katika karama na huyu aliyeandaa karama katika injili walikosa ule utayari na kukazania yao na ndio wakaishia kukosa mwaliko mkuu. Maskini walikuwa na utayari wa kwenda na kufaidi.
Nasi ndugu zangu tukikosa utayari tutaishia kutokushiriki karamu kama hawa waliokuwa wamealikwa. Wengi wetu tumeshindwa kutumiwa na Mungu kwa sababu ya kukosa utayari. Na wengi tumekosa neema nyingi kwa Mungu. Hata baadhi yetu tukifaulu kidogo darasani tunaishia kusema siwezi kujiunga na utawa-nimefaulu mno, nataka niwe daktari. Hapa ni namna mojawapo ya kukosa utayari. Au pale baadhi tunasema kama nina uwezo, sitaki kusoma masomo ya dini, nataka nisome 'secular'-hapa kweli ni kukosa utayari.
Hata kanisani wale wenye uwezo tunakataa kuhudhuria misa jumapili na kuwaachia maskini waende kanisani na sisi tunaendelea na biashara hadi jumapili. Hapa ni kukosa utayari. tungekuwa na utayari hakika tungebarikiwa zaidi.
Mungu hufanya kazi na wale walioko tayari. Maskini wako tayari wakati wowote kwa sababu hawana cha kushikamana nacho. Walio na mali wanakosa utayari, kila kitu wanaona ugumu kujitoa kwa Mungu; kumpatia Mungu muda fulani bado wanaona shida.
Tutambue kwamba pale tunapoanza kuwa wachoyo kwa Mungu ndio mwanzo wa kuanguka. Hawa walioalikwa wamekuwa wachoyo na kukosa ukarimu na utayari kwa ndugu zao na huu ndio ukawa mwanzo wao wa kuanguka. Sisi tubadilike. Tuwe na utayari. Utayari utatufanya tuchanue zaidi.
Maoni
Ingia utoe maoni