Jumamosi, Oktoba 31, 2020
Jumamosi, Octoba 30 , 2020,
Juma la 30 la Mwaka wa Kanisa
Flp 1: 18-26;
Zab 42: 2-3, 5;
Lk 14: 1, 7-11
KUWA WA KWANZA!
Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo katika adhimisho la Misa Takatifu. Zaburi yetu ya wimbo wa katikati leo inatuambia kwamba nafsi yangu inakuonea kiu ee Bwana. Hii kweli ni sala ya mwenye imani; aliyekwisha kuuonja wema wa Bwana na hivyo hataki kutengwa naye kabisa.
Huyu mtu ni Paulo anavyojieleza katika somo la kwanza. Yeye basi anatoa ushuhuda leo, kaishi hapa duniani katika ulinzi mkali kabisa wa Mwenyezi Mungu. Imefikia mahali kuona kwamba hakuna tofauti ya kufa na kuishi. Yote ni mamoja-hii ilikuwa ni dhihirisho kubwa la ukuu wa imani yake. Sisi tuombe kuwa kama Paulo ndugu zangu. Ifikie mahali tuone kwamba maisha ni Kristo, kuishi au kufa yote ni ya Mungu. Wengi hatujafikia hii hali. Hadi ile siku ya kufa tunakuwa na hofu, tunaogopa, tunateseka, ni dhahiri kwamba bado hatujajikabidhi mikononi mwa Mwenyezi Mungu na ndio tunaogopa. Hata baadhi ya wazee wa miaka tisini wataogopa na mwishowe tunakuwa katika hofu.
Tuombe Mungu leo tuachane na hofu hii, tujikabidhi mikononi mwake Mungu. Mungu atosha kabisa.
Kwenye injili Yesu anapinga watu kukaa kwenye viti vya mbele, kujitangazia utukufu wenyewe kabla ya watu kuwatangazia huu utukufu, kujiita watakatifu kabla ya kutangazwa. Yesu kwa hapa anakataza tabia ya kungangania mambo; kungangani ni dhihirisho la hofu ndani ya roho ya mtu, dhihirisho la kukosekana kwa imani, kutokujiamini kwamba nafasi yako itabakia na hivyo unaanza kuwahi mapema.
Lakini anayejiamini hataanza kwa kuwahi kwani anajua kwamba nafasi yake ipo tu. Na huyu anayeanza kwa kukaa kwenye nafasi ya mbele huishia kukosa kila kitu kwani atakapokuwa ananyanyuka kurudi, atakuta hata ile nafasi ya nyuma imekwishachukuliwa na wengine na ataishia kusimama. Ndivyo inavyotokea na kwetu sisi pale tunapoanza kujiita watakatifu-tunaishia kukosa kila kitu kwani wakati tunapohukumiwa na kuambiwa kwamba hatufai, unakuta hata ile nafasi ya kutubu haipo tena kwani muda unakuta umekwisha na tunaishia kutupwa motoni.
Ukingangania nafasi ya mbele unaishia kujisahau na kutoitambua hali yako na huishia kuanguka zaidi. Leo tuangalie jinsi nafasi ya mbele inavyoangusha, jinsi ilivyotufanya tuwadharau wenzetu, tuwanyanyase wenzetu na kusahau kutubu.
Maoni
Ingia utoe maoni