Alhamisi, Oktoba 22, 2020
Alhamisi, Oktoba 22, 2020,
Juma la 29 la Mwaka wa Kanisa
Ef 3:14-21
Zab 32:1-2, 4-5, 11-12, 18-19
Lk 12: 49-53
MUNGU NI MOTO UNAOPENDEZESHA VYOTE.
Ndugu zangu katika Kristo karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu asuhuhi ya leo. Leo tuanze tafakari yetu kwa kuiangalia zaburi yetu, ambapo tunamuona Mzaburi akituambia kwamba nchi imejaa fadhili za Bwana. Kila kitu kilichopo ulimwenguni pamoja na uzuri wake wote ni mali ya Bwana. Hivyo hizi fadhili za Bwana tuzitumie huku tukijua sio zetu ni za Bwana. Tuzitumie kwa ukarimu tukifahamu kila fadhili ni mali ya Mungu. Yeye hufurahi tunaposhirikisha hizi fadhili bila uchoyo.
Ndugu zangu Zaburi hii inatilia mkazo ujumbe wa Paulo kwa Waefeso, anawaeleza watambue wao wamekuwa wamoja na Mungu ni Baba yao kwa njia ya Kristo. Hivyo wahakikishe wanatiwa nguvu kwa Roho wa Kristo wabaki katika imani moja na tena wakiwa katika shina kuu la upendo. Paulo anamshukuru Mungu kwa zawadi hii.
Ndugu zangu tunajifunza kitu hapa kwamba sisi Mungu ni Baba yetu zote na fadhili zote ulimwenguni ni mali yake. Tusidhulumu wala kujivuna tuongozwe na Roho wa Kristo tena kwa imani tukiwa tumejawa mapendo na wala tusibaguane. Tukifanya hivi kwa kuondoa wivu, na madhulumu yote kila mtu atakiri kweli sisi ni watoto wa Mungu kwa njia ya Kristo.
Katika Somo la Injili Yesu anatupa tahadhari nyingine kwamba kwa ujio wake yaweza kuwa amekuja kuwasha moto duniani. Na hili kweli linatokea nyakati zetu, tumeshuhudia familia zikitengana kwa kigezo cha Injili tena wote wakiwa wafuasi wa Kristo. Wengine hujidai wanamuelewa Kristo zaidi na kuwadharau wengine. Wengine huamka hata usiku wa manane na kuwasumbua wengine kwa sala za kelele kwa kisingizio wanafukuza pepo na kuwafanya wengine wasilale. Wengine hujifanya wafafanuzi wazuri wa maandiko zaidi kuliko wengine na hivyo kuishia kushindana. Yesu haya aliyatambua yatakuwepo. Paulo anatupatia jibu zuri sanaa katika somo la kwanza, hamna namna nyingine ya kuonesha kwamba sisi ni wafuasi wa Kristo isipokuwa kwa njia ya upendo. Utengano sio sifa ya Kristo.
Tusitumie pia sala kama kisingizio cha kuwakashifu wale wasio sali. Tusijione wema zaidi kwasababu tu sisi tunaenda kanisani na wengine hawaendi. Badala yake sisi tuwaombee waregevu na kuwashauri kwa upendo na upole ili waweze kuvutwa nao kumtumikia Kristo. Tusiwashe moto duniani wa fujo kwakutumia Injili ya Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni