Jumanne, Oktoba 27, 2020
Jumanne, Oktoba 27, 2020,
Juma la 30 la Mwaka wa Kanisa
Ef 5: 21-33;
Zab 128: 1-5;
Lk 13: 18-21
UFALME WA MUNGU-UPO NA BADO UTAKAMILIKA
Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu katika adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi tafakari yetu inaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati ambapo tunamkuta mzaburi akielezea juu ya faida atakayoipata yeyote yule amchaye Bwana. Familia yake itakuwa na utulivu na yeye atafurahia kuishi ndani yake.
Hapa twajifunza kwamba kumcha Bwana ndio chanzo cha baraka ndani ya familia na kinachokusaidia ufurahie kuishi ndani ya familia. Baadhi yetu kwa siku zetu hizi hatufurahii maisha ndani ya familia zetu, tunapata raha zaidi tukiwa nje ya familia kuliko tukiwa ndani. Familia inakuwa kama gereza. Tuanze kwa kumcha Bwana na maisha ndani ya familia yatavutia zaidi.
Tumemtupa Bwana, tumeacha kusali pamoja na hiki ndicho chanzo cha chuki ndani ya familia. Hata fundisho linaloelezewa na Paulo katika somo la kwanza linaeleweka kwa familia inayosali. Familia inayojali sala ndiyo inayoweza kuishi maisha ya utulivu na kutumikiana, ya mke kumtambua mume wake kama kichwa cha familia na ya mume kumwona mke wake kama sehemu ya mwili wake. Bila sala ndani ya familia hili fundisho halieleweki. Tukizidishe sala hili litakuwa fundisho rahisi. Sala huifanya familia ipendeze, ivutie, iwe kama ua. Tuzidishe sala ndani ya familia zetu.
Katika injili Yesu anatumia mfano wa punje ya haradali na chachu kuelezea namna ufalme wa mbinguni unavyoanza kwa mambo madogo madogo na kuweza kupanuka na kuwa makubwa zaidi.
Familia ni kiungo muhimu kwa maisha ya mkristo yeyote. Tukizijenga familia zetu kwa sala, kila mmoja wetu akifanya hivyo ama kweli tutamjengea Mwenyezi Mungu ufalme mkuu kabisa. Familia zetu ndio kitalu cha ufalme wa mbinguni. Tujitahidi imani, utulivu, furaha, amani vifunike familia zetu. Huu utakuwa mchango mkubwa sana katika uinjilishaji.
Pia yote aliotupa Mungu iwe ni kipaji au chochote hata kama tunaona ni kidogo tukitumie kwa upendo utashangaa kitakuwa, na sisi wenyewe tutasitawi na wengine watapata kivuli chini ya kile tulichokikuza kwa upendo alichotupatia Mungu.
Maoni
Ingia utoe maoni