Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Oktoba 24, 2020

Jumamosi, Oktoba, 24, 2020,
Juma la 29 la Mwaka wa Kanisa


Ef 4:7-16;
Zab 121:1-5;
Lk 13:1-9


THAMANI YA WAKATI WA SASA!

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Bwana katika adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi Paulo anawaeleza Wakristo wa Efeso kwamba Kristo aliposhuka kuzimu na baadaye kupaa, aliweza kuwakweza wanadamu ndani ya Kanisa. Wakristo tulipata nafasi kupokea vipaji mbalimbali: wengine tukifanywa waalimu, wengine mitume, wengine waenjili. Vyote hivi ni zawadi tosha toka kwa Mungu. Kila mmoja alimpatia kipaji na hadhi yake, alimwimarisha ili basi asipeperushwe tena na upepo. Hivyo tunapaswa basi kusimama imara, tujiamini; Kristo ametupatia uwezo na hadhi kubwa na katika Lk 10:29, anasema kwamba ametupatia uwezo wa kukanyaga nge na nyoka.

Wengi tunashindwa na shetani kwa sababu hatujiamini. Shetani ametuonea sana, hatuamini kwamba Kristo ametupa uwezo, hata tunapokuwa katika kuadhimisha mafumbo matakatifu-tunasema baadhi yetu je, hivi vitu ni kweli? Tutambue kwamba tukishindwa kujiamini, basi ndio mwanzo wa sisi kushindwa kwa mengi. Tujiamini ndugu zangu ili tumpatie sifa na shetani asitutese tena. Shetani anatabia ya kutufanya tusijiamini, tujisikie kwamba hatuna uwezo na hili linatufanya tushindwe kwa mengi na kurudi nyuma. Tusikubali kurudi nyuma kila siku.

Katika somo la injili Yesu anatoa mfano wa walioangukiwa na mnara na kufa kifo kibaya na kufundisha kwamba haimaanishi hawa wanaopatwa na mkasa huu ndio wadhambi.

Wakati mwingine sisi tunaobaki ndio wadhambi zaidi. Kile kipindi cha sisi tunabakia bila kuadhibiwa na tunabakia kusikia na kuona maumivu ya wengine ni kipindi cha kutufunza ili tuache dhambi. Ajali za wengine na mateso yao unayaona kwenye tv, au wakimbizi wakilia yote haya ni nafasi zitutakazo tuongeze bidii tuweka samadi ya kiroho. Ni kipindi ambacho tunatiliwa samadi kama huyu mkulima anavyofanya kwa huu mti wake ili tubadilike na tusipobadilika tutakatwa.

Wadhambi wengi tunaendelea kuishi kwa sababu ya huruma ya Mungu. Kati yetu tunaishi na watu ambao labda tungaliomba wawe wamekwishaadhibiwa tayari lakini Yesu anaruhusu waendelee kuishi ili basi wabadilike, ni huruma ya mkulima. Sisi tubadilike na tukiona hatujaadhibiwa tusijione ati sisi ni wajanja sana au Mungu hana nguvu. Mungu akiamua, nakueleza sisi hatutasalia. Tuombe kutumia nafasi tupewazo vyema. Wengi tunatumia vibaya kile kipindi Mungu anapokaa kimya na kuamua kumtukana na kumwona kana kwamba hana nguvu. Kwa hapa tunajilaani zaidi. Mungu ni mkuu kila wakati. Tuache kumkosea adabu.

Maoni


Ingia utoe maoni