Jumatatu, Disemba 05, 2016
Jumatatu, Desemba 5, 2016,
Juma la 2 la Majilio
Isa 35:1-10
Zab 85: 9-14
Lk 5: 17-26
JE UNATAMANI KUPONYWA?
Katika Injili ya leo, tunamwona Masiha akitimiza yale yale aliotabiri nabii Isaya katika somo la kwanza leo, akitoa matumani mapya kwa wagonjwa na kuwaponya na kuwafanya warukeruke tena kwa furaha. Katika Injili tunaona uponyaji wa mtu aliyepooza katika hali ya Imani ya hali ya juu. Huyu mgonjwa hakuwa anajiweza na alihitaji msaada wa kubebwa na mkeka na kuletwa kwa Yesu. Hawa marafiki walipata vipingamizi kabla ya kumfikisha kwa Yesu kwa msaada. Kulikuwa na hali ya kukatisha tamaa walipofika katika nyumba ile, lakini hawakukata tamaa. Wanapanda juu ya paa, na kuondoa paa na kumshusha alipokuwa Yesu. Injili inaeleza wazi kwamba ‘Yesu baada ya kuona Imani yao’. Huyu mgonjwa hakumtafuta Yesu mwenyewe, Imani yake kwa Bwana ilisaidiwa na imani ya wenzake. Umoja wao ulifanikisha. Yesu anamponya huyu mgonjwa na anamsamehe dhambi zake. Hapokei uponyaji tu wa mwili bali uponyaji mkamilifu wa kuondolewa dhambi zake zote.
Tutafakari leo juu ya hamu yetu ya kupokea Msamaha wa Mungu katika maisha yetu. Je, unatamani kupokea huruma ya Yesu na msamaha wake katika maisha yako? Sababu ya Yesu kuja ulimwenguni kutoka mbinguni ni kutusamehe dhambi zetu na kutupatanisha na Mungu Baba. Miujiza mikubwa sio kigezo, kigezo ni msahama. Utakapo pokea zawadi hii ya huruma na msamaha, utamtukuza pia Mungu kwa furaha. Tunaomba kipindi hiki cha majilio kilete furaha mpya katika maisha yetu kwa msamaha wa Mungu.
Sala: Bwana, natamani huruma na msamaha katika maisha yangu. Nisaidie Bwana nijishushe mbele yako ili niweze kusikia ukisema ‘dhambi zako zimesamehewa’. Yesu nakuamini wewe. Amina
Maoni
Ingia utoe maoni