Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Oktoba 21, 2020

Jumatano, Oktoba 21, 2020,
Juma la 29 la Mwaka wa Kanisa

Ef 3:2-12;
Is 12:2-6;
Lk 12:39-48


UFUASI: WITO WA KUWA MWAMINIFU, SI KWAAJILI YA MAFANIKIO!

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Bwana katika adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi tafakari yetu inaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati ambapo tunakutana na mzaburi akishangilia kwamba kwa furaha tutateka maji katika kisima cha wokovu. Hii ni sababu yake yeye kushangilia. Mzaburi anadiriki kusema hayo yote kwasababu anaona kwamba neema zote na baraka anazopokea Israeli ni upendeleo wa pekee. Mara nyingi Israeli amekuwa mkaidi lakini Mungu alizidi kumpatia neema. Hivyo basi Mzaburi anakiri kwamba atahakikisha kwamba kila siku atamtukuza Mungu kila wakati na sifa zake zitabakia kinywani mwake daima.

Zaburi hii inatuunganisha vyema na somo la kwanza. Leo Paulo anasema kwamba hata yeye na Waefeso wote wamepata baraka na upendeleo wa kufunuliwa siri ya Bwana-siri ya kwamba Kristo ndiye anayewaokoa wote na hivyo wamwamini Kristo wapate wokovu. Huyu Kristo aliwakomboa kwa kumwaga damu yake msalabani. Kila anayemkiri Yesu kuwa ni mwana wa Mungu atapata wokovu. Kristo ameondoa uadui kati ya makabila, rangi, tabaka na elimu zetu. Hii ni siri kuu ambayo basi wengi hawakuifahamu na hii ilifunuliwa kwa wale walioiamini injili tu. Paulo anawaeleza Waefeso kwamba wanayokila sababu ya kumshukuru Mungu kwa wao kufunuliwa matendo makuu na siri kuu namna hii kwani wengi hawaijui. Wao wamshukuru Mungu. Ni upendeleo wa karibu.

Somo hili ni mwaliko kwetu ndugu zangu wa kutambua kwamba hata sisi tayari tumebarikiwa na Bwana vya kutosha. Baadhi mwanzoni tulikuwa maskini kabisa lakini sasa Mungu ametusaidia kupandisha kipato chetu. Wengine tulikuwa tunaburutwa kwenye masomo lakini sasa basi Mungu ametuweka juu. Wengine tumepandishwa vyeo na sasa ni watu wakubwa kabisa. Tunapaswa kumshukuru Mungu kwa hili ndugu zangu. Tuone kama nafasi ya upendeleo, tusijivune bali tushirikishane na wengine hizi neema za mwenyezi Mungu.

Katika injili Yesu anazungumzia ujio wa nyakati za mwisho na anasisitiza kwamba siku hiyo itakuwa ni siku ya watu kutoa hesabu. Kuna wale waliokabidhiwa mengi na hivyo watadaiwa mengi toka kwao pia. Sisi ndugu zangu tujiangalie ni mangapi tumekabidhiwa? Namna gani tumetumia kwenye kuwasaidia wenzetu au kuwatesa. Tusitumie ujuzi wetu au cheo au pesa au maarifa kwenye kuwadanganya wenzetu. Wengi tumetumia maarifa yetu kuwadanganya wenzetu, tumetumia mbinu kuwaibia fedha zao au kushinda kesi kwa ujanja wetu na kuishia kuwadhulumu. Hapa tutadaiwa mengi.

Tusiwadanganye walio wadogo. Wasiojua lugha au kisomo tusiwatafsirie vitu vya uongo. Huku ndiko kukesha atakakotukuta Yesu tukiwa tayari kumlaki na yeye atatuhudumia na kutupatia nafasi ya pekee katika ufalme wake.

Maoni


Ingia utoe maoni