Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Oktoba 20, 2020

Jumanne, Oktoba 20, 2020
Juma la 29 la Mwaka

Efe 2:12-22
Zab 85: 9-14;
Lk 12: 35-38.

KUWA MWEPESI KUMKARIBISHA YESU

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Bwana katika adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi tunaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati ambapo tunamkuta Mwenyezi Mungu akiwatakia amani watu wake.

Paulo katika somo la kwanza anaendeleza msemo huu wa amani kwa kusisitiza ukweli kwamba amani ya kweli imeletwa na Kristo mwenyewe. Ndiye aliyeteseka na kufuta uadui uliokuwa baina ya mwanadamu na Mungu na hata baina ya wanadamu na wanadamu. Amekomesha uadui uliokuwa kati ya Wayahudi na watu wa mataifa na kuwafanya kuwa kitu kimoja. Ndiyo maana tukikutana kama wakristo, lugha yetu lazima iwe ya Kristo-makabila, rangi, kisomo, urefu au ufupi vyote huisha. Lugha yetu hubakia kuwa moja yaani ya Kristo.

Lakini kwa bahati mbaya tumeshindwa katika hili. Bado tunashuhudia wabatizwa wakiishi katika uadui mkubwa-wakati mwingine makabila yameonekana kuwa ya maana zaidi kuliko hata ukristo wetu. Tumeshuhudia wakristo wakifanyiana visa vikubwa na wengine kuuana bila kujali kwamba mwenzake ni mbatizwa. Yote haya ni ukiukwaji wa ukristo wetu na imani yetu.

Tumeshuhudia wakristo hata wakitengana-tumekubali kuona wenzetu wanakufa njaa mbele ya macho yetu na sisi hatufanyi kitu na bado tunajiita Wakristo. Lazima tubadilike tuishi ukristo wetu. Umoja unaoletwa na Kristo utatusaidia sana zaidi ya ule umoja tunaofikiri utaletwa na makabila, rangi, lugha au tabaka letu. Tukimkumbatia Kristo tutafaidi zaidi. Tumkumbatie Kristo.

Huku ndiko kukesha kunakoelezewa katika injili ya leo. Yesu anataka akija atukute tuko kama watumishi wanaowatumikia wenzao na kweli akija atatupa tuzo. Lakini akitukuta katika hali ya kutengana na kunyanyasana kwa makabila au watu wa tabaka za chini. Akitukuta katika ubinafsi wa kuwanyonya wengine kana kwamba hao sio binadamu au katika hali ya kutokujali-hakika atatuadhibu vibaya sana.

Kukesha ni kuwatumikia wenzetu. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni