Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Oktoba 19, 2020

Jumatatu, Oktoba 19, 2020,
Juma la 29 la Mwaka wa Kanisa

Ef 2:1-10
Zab 100:2-5
Lk 12:13-21


KUWA TAJIRI KUMWELEKEA MUNGU!

Karibuni ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu ya neno la Bwana inaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo Paulo anawaeleza Waefeso juu ya upendo wa Mungu kwa njia ya Kristo:kwamba wamepata bahati zaidi ya wenzao. Wao wamekombolewa toka katika maisha yasiyofaa kwa damu takatifu ya Kristo. Hivyo basi wajifunze kutambua upendo na ukuu huu wa Kristo.

Waefeso wanaambiwa hivi kwa sababu baadhi yao walianza kulegalega na kuanza kutamani maisha waliyoishi wale wapagani wakifikiri kwamba wanafaidi zaidi. Hivyo walishindwa kuona nguvu ya Kristo maishani mwao. Paulo anawaambia wamkumbatie Kristo ili basi waweze kuiona nguvu yake maishani.

Ndugu zangu, kilichowatokea Waefeso kinazidi kututokea na sisi kila siku. Wengi wetu tunashindwa kuiona nguvu ya Kristo kwa sababu bado tunatabia ya kutamani maisha mengine-tunafikiri kwamba wanaoishi maisha yasiyo na Kristo wanafaidi zaidi. Tamaa ya namna hii imetukosesha mengi katika uhusiano wetu na Kristo. Tamaa zinatufanya tuwe wachoyo wa kumpatia Mungu nafasi yake. Tunashindwa kutoa hata kasehemu kadogo ya muda wetu hata kasehemu sifa yetu kwa ajili ya Kristo. Sisi tuzidi kumkumbatia Kristo naye atatuonyesha nguvu zake maishani mwetu zaidi na zaidi.

Mfano mzuri wa tamaa tunakutana nao leo katika injili yetu. Tajiri huyu alizidisha tamaa-akawa mchoyo wa kumpatia Mungu hata kasehemu cha sifa kwa kumwezesha kufanikisha mazao mengi hivyo. Kama angalimpatia Mungu nafasi yake, asingalikuwa na cha kupoteza lakini tamaa zilimfanya aone shida hata kuzungumza neno moja amshukuru Mungu. Hii iliyomtokea huyu tajiri inatutokea na sisi kila siku. Sisi tunapoteza mengi kwa sababu ya kuona ugumu kutumia hata dakika tano kumshukuru Mungu-yaani dakika tano tu. Sio zaidi. Tunapewa masaa yote 24 kwa ajili ya shughuli zetu tu lakini dakika tano za kumrudishia Mungu tunaona shida.

Tunaishia hata kukosa kanisani jumapili ili tuzalishe mali. Hii sio sahihi. Lazima tubadilike ndugu zangu. Wengi wetu ni maskini na tumenyanganywa mengi kwa sababu ya kukosa kuwa na shukrani tu. Ndio hiyo tu. Tunapata milioni moja lakini tunaona ugumu kutoa hata shilingi elfu kumi umpatie Mungu shukrani. Jamani! Hapa hatujafanana na huyu tajiri? Tunapokea mshahara wa laki nne lakini maskini akija akiomba hata hapo miatano tunakataa. Tubadiilike yasije yakatutokea yaliyomtokea huyu tajiri.

Tunashuhudia watu wakikazana kutafuta mali kila siku asubuhi na mchana ili wawe nazo lakini wanaondoka na kuziacha bila ya wao kutumia kitu chochote-au wanaziacha kwa watoto wao ambao huzitapanya na kuishia hivihivi tu. Au zile mali zinakuja kupotea potea na kutumiwa hata na watu ambao hata hapo mwanzo hawakuzifanyia kazi. Matukio yote haya yatufanye tubadilike.

Maoni


Ingia utoe maoni