Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Oktoba 17, 2020

Jumamosi, Oktoba 17, 2020,
Juma la 28 la Mwaka wa Kanisa

Ef 1: 15-23;
Zab 8: 2-7;
Lk 12: 8-12.

IMANI ILIYO JARIBIWA!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi Paulo anaandika sehemu ya barua ya kwa Waefeso panapotoka somo letu la kwanza leo katika lugha ya utulivu kabisa na matumaini. Anamshukuru Mungu jinsi Waefeso walivyomuweka Mungu mbele na anawombea, na anazidi kuwaeleza juu ya nguvu ya Kristo na jinsi alivyoviweka vitu vyote chini ya miguu yake.

Inamlazimu Paulo atoe maelezo marefu juu ya nguvu ya ukuu wa Kristo kwa sababu Waefeso waliishi katika jumuiya waliposhambuliwa na Filosofia na nguvu nyingine za kisiri. Paulo anawatia moyo kwamba Kristo ananguvu na ndiye wa kutumainiwa.

Jibu la namna hii tunalihitaji kwa nyakati zetu hizi pia. Wengi wetu tunashindwa kuziona nguvu za Kristo; Kristo ni rasilimali kubwa sana. Wengi wetu tumerudi nyuma kwa sababu tunamuona Kristo kana kwamba hatoshi; tuombe kuwa na imani zaidi. Kristo anatosha.

Katika injili Yesu anasema kwamba anayemkana mbele ya watu naye pia atamkana mbele ya Babaye. Tunamkana Kristo pale tunapomuona kana kwamba hatoshi maishani mwetu. Kila siku tunamkana Kristo kwa pale tunapoona aibu kusali mbele za watu au pale tunapowaona kama washamba wale wanaopendelea masuala ya kiroho. Tunawaona washamba. Mtu akivaa rozari anaonekana kwa baadhi ya watu kama ni mshamba zaidi ya yule aliyevaa licheni la dhahabu lililochorwa labda mnyama. Huyu aliyevaa hili licheni tunamuona kuwa mjanja zaidi. Hapa ni kumkana Kristo hadharani.

Au kwa pale unakuta mabaa au viwanja vya mipira vimejaa kuliko kanisa. Hapa ni kumkana Kristo hadharani. Au kukuta kwamba watu wanaovaa nguo panapana na za heshima tunawaona kama waliorudi nyuma zaidi ya wale wanaovaa vimodo vyembamba na vyakubana. Hapa ni kumpatia shetani nguvu na kumdidimiza Kristo.

Tuache kumdidimiza Kristo ndugu zangu.
Kama wimbo wetu wa katikati unavyotuongoza leo, tutambue kwamba Mungu anapaswa kusifika na vinywa vya watoto na wote; tumpatie muda na kumtagaza. Macho yangu yanapoona ya kishetani zaidi kuliko ya kimungu ni dhahiri kwamba ninamkana Kristo hadharani. Tumweke Kristo mbele.

Yesu katika injili anasema tusiogope kwa pale tupelekwapo mikononi mwa maadui zetu. Kila mmoja wetu aondoe aibu na hofu inayomzuia asiwe chombo kiteule cha Kristo kinachomshuhudia. Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni