Ijumaa, Oktoba 16, 2020
Ijumaa, Oktoba 16, 2020,
Juma la 28 la Mwaka wa Kanisa
Ef 1:11-14;
Zab 32:1-2, 4-5, 12-13;
Lk 12:1-7
KUTANGAZA INJILI BILA WOGA!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi neno la Bwana linaanza kwa kuiangalia injili yetu ambapo tunakutana na Yesu akiendelea kuwaeleza ukweli wa maisha ya viongozi wa Kiyahudi hasa Wafarisayo.
Anapowaona Wafarisayo, moja kwa moja anawaeleza wanafunzi wake kwamba wajiepushe na unafiki. Anawaeleza dhahiri kwamba wakati utafika kila kitu kitafunuliwa, hata kile wanachofikiri kwamba kimefichika sana. Hivyo, waepuke kufanya vitu kisirisiri vibaya halafu wanaonekana wema kumbe ndani yao ni watu waovu. Hili ndilo lililowafanya Wafarisayo wasiweze kutoa uponyaji kwa yeyote; zamani za Yesu walikuwako Wafarisayo wengi lakini walishindwa kuyagusa maisha ya watu kutokana na unafiki-hawakuweza kuwagusa yatima, wajane au wenye magonjwa. Yesu aliweza kwa sababu alipinga unafiki.
Kila mmoja wetu anayo chembe ya ufarisayo moyoni mwake. Hivyo yatupasa tupambane na unafiki wetu. Kila mmoja wetu leo achunguze ni kitu gani anachoficha, ni vitabia gani alivyonavyo anavyotenda kisirisiri. Na hivi vinamrudisha vyuma. Yesu leo anakuambia kwamba viache vitabia hivyo, maisha yako ya kisirisiri nawe utakuwa huru na mlango wa baraka za Mwenyezi Mungu utakufungukia zaidi na zaidi. Woga na kutaka kutokuwachukiza wenzetu ndio labda kwa wakati mwingine unatufanya tuzidishe unafiki. Lakini Yesu anasema tusiogope wale wawezao kuua mwili tu. Tusiogope hao. Sisi tumweke Mungu mbele zaidi.
Sisi ni jukumu letu kufanya hivi kwani katika somo la kwanza Paulo anatuambia kwamba tumempokea Roho Mtakatifu na huyu Roho tuliyompokea toka kwa Kristo. Tuishi maisha huru; tusiogopeshwe na vitu kama urafiki au mengineyo yote-tujikabidhi mikononi mwa mwenyezi Mungu naye atatuweka kuwa huru zaidi na zaidi.
Maoni
Ingia utoe maoni