Jumatano, Oktoba 14, 2020
Jumatano, Oktoba 14, 2020,
Juma la 28 la Mwaka wa Kanisa
Gal 5:18-25;
Zab 1:1-4, 6;
Lk 11:42-46
KUJIZOESHA KUTENDA FADHILA!
Karibuni ndugu zangu kwenye tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Leo basi neno la Bwana linaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati ambayo inasisitiza juu ya faida ya yule aichaguaye njia ya Bwana-huyu hujiletea faida maishani mwake, maisha yake huwa na baraka, Bwana humpatia virutubisho kama mti ulioko kwenye vijito vya maji unavyorutubishwa.
Katika somo la injili, tunagundua kwamba wafarisayo walikosa virutubisho toka kwa Bwana na Yesu anaishia kuwaita kwa jina baya kabisa-wanaonekana kama makaburi ambayo yaliyojaaa na uozo lakini kwa nje yanaonekana kama yaliyopambwa vizuri sana.
Ndugu zangu, hii ni sifa mbaya sana kwa hawa wafarisayo na kweli kama walikuwako karibu kweli waliumbuliwa vibaya sana kwa neno hili. Yaani walikuwa wanafiki wa hali ya juu, kuficha mambo, kuonekana kwa watu kuwa ni wema lakini kumbe kwa ndani walikuwa ni watu wabaya sana. Na ukweli kwamba wale watu wa namna hii hukwaza watu kwa kiasi kikubwa sana-unakuta wanaheshimika sana, wanasifiwa vizuri, hata watu wanawapeleka watoto na ndugu zao wakafundishwe nao lakini sasa wanapokuja kutambua kwamba kuna matendo ya siri yanayoendeshwa chini chini na hawa watu wanaopewa heshima hivi huishia kudharaulika kabisa.
Sisi ndugu zangu wengi wetu tunatabia ya kuficha mambo ili tuonekane wema. Kama tumeishi kifarisayo kwa miaka yote hiyo na kuweza kuwadanganya watu kwamba tu wema, basi cha kufanya leo ni kubadilika tu, kuishi ule wema tunaouonyesha kwa nje. Kila mmoja ajione kwamba anayemfuasi anayemuona yeye kuwa kama kioo kwake, na hivyo basi aone huzuni kumkwaza. Ukweli ni kwamba tuna dhambi nyingi sana za kuwakwaza wenzetu kwani mara nyingi tunatabia ya kutenda bila kufikiri kwamba kuna wanaotutazama. Hivyo hata katika sala zetu, ni lazima tuombe msamaha kwa kuwakwaza wenzetu hasa wale waliowadogo.
Tukijikabidhi kwa Mungu kila siku, tukija kwake na kuomba neema zake kwa kila siku hakika tutaepuka dhambi hizi za makwazo kwani Mungu atatuongoza na hakika tutaona hasara za dhambi za makwazo na kuacha kujifichaficha ili tuonekane wema. Wengi wetu tunakwaza kwa sababu ya kuacha kusali, mioyo yetu inakuwa migumu na kushidwa kuona hasara ya matendo yetu kwa wengine tuongozwe na Roho kama Paulo anavyotuambia katika somo la kwanza.
Maoni
Ingia utoe maoni