Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Oktoba 13, 2020

Jumanne, Oktoba 13, 2020,
Juma la 28 la Mwaka wa Kanisa

Gal 5:1-6
Zab 118:41, 44-45, 47-48
Lk 11:37-41

YESU ANAYASEMA YOTE KWA UWAZI

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Bado tunaendelea na waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia na leo bado Paulo anaongelea kuhusu uhuru wa kweli unaoletwa na Imani yetu ndani ya Kristo tena kwa njia ya Upendo. Kuwa mtumwa wa sheria isiyo jaa mapendo ya Kristo inatufanya sisi tuwe watumwa. Na hili ni kweli katika maisha yetu tumeona watu wengi wanaongangania kushika sheria mno bila mapendo hufanya wengine wateseke kwani wanaishi kwa hofu bila kujali utu na hivyo huishia kusisitiza sheria tuu. Mfano waweza kukuta sheria inasisitiza kuwahi kazini asubuhi lakini mmoja anaposhindwa kuwahi kwasababu ya ugonjwa wake ni lazima hapo sheria iwe na mapendo ya kutazama afya yake, na sheria inapojali utu wa watu zaidi hii ndiyo sheria ya mapendo ambayo Kristo ametufundisha ndugu zangu. Unapokosa mapendo utataka kutenda mambo kujali mambo ya nje tuu na kulinda sifa yako na hutajali wengine.

Dhana kama hii tunaiona katika somo la Injili, tunapokutana na Yesu akishutumiwa kwa kula chakula bila kunawa mikono na kushika mapokeo ya Wayahudi. Yesu anawaonya Mafarisayo juu ya unafiki wao. Wao hujionesha kwa nje kwamba ni wasafi lakini moyoni mwao kuna uozo mkubwa. Ndugu zangu nasi tunaonywa kuhusu unafiki, kuonesha taswira tofauti mbele za watu wakati moyoni Mungu yupo mbali sana. Tumeteseka sana kuwafurahisha wanadamu, na kutaka kuonekana wazuri machoni pa watu kumbe tuna dhambi za sirisiri na hizi ndizo zitatutafuna na kutunyima Mbingu.

Hili ni fundisho kwa viongozi mbali mbali katika kanisa, au sehemu yeyote tuangalie sana tusije kuwa kama Mafarisayo. Tumekuwa tukisisitiza sana kuhusu kushika sheria lakini pengine sisi wenyewe mioyo yetu ipo mbali mno na Mungu. Tunasimama mbele pengine tunatoa matangazo kanisani, tena kwakuweka sauti nzuri kama malaika na kutaka kuwaonesha watu kwamba sisi ni wazuri sana, lakini ukweli ni kwamba mioyo yetu ipo mbali mnoo. Tumeridhika na vigelegele vya watu tukasahau ukweli wetu wa mioyo yetu mbele za Mungu. Utakatifu wa kwanza kabisa ni wewe kuwa uhusiano mzuri na Mungu.

Tunafanya kazi nzuri kanisani, pengine kutoa michango mingi na kusifiwa, kupigiwa makofi na kuvimbishwa vichwa, kumbe ndugu zangu, tunaongoza kwakuwa na nyumba ndogo, kurukaruka na vibinti vya watu, au waume wa watu au kusujudu miungu mingine. Tafakari juu ya dhambi zako za siri ambazo unazifahamu wewe na Mungu. Hizo zitakukosesha Mbingu. Bora uonekane vibaya machoni pa watu kuliko Mungu kukuona huna wema moyoni. Tujitahidi kuacha unafiki ndugu zangu tukazane kuosha roho zetu ziwe safi na hata matendo ya nje yatakuwa safi. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni