Jumatatu, Oktoba 12, 2020
Jumatatu, Oktoba 12, 2020,
Juma la 28 la Mwaka wa Kanisa
Gal 4:22-24, 26-27, 31 - 5:1;
Zab 112:1-7;
Lk 11:29-32
UHURU WA KWELI NDANI YA YESU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi neno la Bwana linaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na ujumbe wa Paulo kwamba sisi wakristo sio wana wa utumwa; tumepewa hadhi kubwa sana na Bwana wetu Yesu Kristo na hivyo tunapaswa kuishi kama wana huru.
Yesu amekwishatuokoa kutoka utumwani mwa shetani, alikwishateseka na kumwaga damu yake na kutupatia hadhi na hivyo tuko huru. Tuishi kama watu huru. Sasa, tujiangalie ni kwa namna gani tunashindwa kuishi kama watu huru. Tujiulize ni kwa namna gani tunashindwa kuishi kama watu huru? Pale tunapokubali kuwa wachoyo wa kumsifu Mungu-na kushindwa kumpatia Mungu nafasi ya kumsifu, tukakubali kutumia muda wote tukamwacha Mungu pembeni, tukabanwa na baadhi ya vitu kama biashara, marafiki, ulevi tukashindwa kutoa muda kwa ajili ya Yesu; au tukakubali vitu kama masomo vitubane tukashindwa kumpatia muda hata kidogo. Pale tunaposhindwa kumpatia Mungu muda, tujue kwamba ndio mwanzo wa maanguko yetu; uhuru wetu unatunzwa kwa njia ya sala-kuacha kusali ndio sababu za kuwa mtumwa na wengi tunaanguka kwa sababu tunaacha sala na pale tunarudi tena na kuwa watumwa. Tuthamini sana na tutunze mafanikio yetu kwa njia ya sala.
Kwenye somo la Injili tunamkuta Yesu akihuzunika kwa sababu ya watu kukosa imani na kutaka ishara na wakati hawana imani. Yesu alihuzunika kwa sababu watu hawa walitaka ishara na hawana imani. Ishara ni kwa ajili ya wale walio na imani, hadi leo, unashangaa kuona kwamba wale wenye imani ndio wanaopewaga ishara ili ziiimarishe imani yao. Wasiokuwa na imani hawataweza kupewa ishara kwani ishara hii haitawasaidia kitu. Sisi tuombe kuwa watu wa imani.
Kingine pia tuwe watu wa kuridhika, baadhi ya viongozi wa Wayahudi walikuwa watu wa tamaa na kukosa kurithika. Walikuwa wamekwishapewa ishara nyingi lakini wakashindwa kuzitumia na hivyo wanahitaji zaidi. Kila mmoja anapaswa kujichunguza leo na kuona kwamba ni ishara gani na zipi Mungu alikwisha mpatia maishani, vitu kama ugonjwa, kupata kazi, kushinda mtihani ni ishara tosha. Tuzitumie kumfahamu na kumtukuza Mungu zaidi. Turidhike na kile tupewacho na tukitumie hicho kwanza.
Wanafunzi wengi hufeli mtihani kwa sababu ya kutokujiamini uwezo wao. Wanaishia kwenda kuibia kwa wenzao wakifikiri kwamba wanao uwezo zaidi yao kumbe wakati mwngine sio hivyo. Sisi tuache kwenda kuibia ibia makanisa mengine tukifikiri kwamba kuna uwezo zaidi, turidhike na tulichonacho kwanza kwenye kanisa letu. Tuache kuhamahama kutafuta ishara.
Maoni
Ingia utoe maoni