Jumamosi, Oktoba 10, 2020
Jumamosi, Oktoba 10, 2020,
Juma la 27 la Mwaka wa Kanisa
Gal 3: 22-29;
Zab 104: 2-7;
Lk 11: 27-28
KUBADILI MAVAZI!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi naomba tafakari yetu ianze kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na maneno kwamba sote tuliobatizwa katika Kristo tumemvaa Kristo, tunakuwa uzao wa Abrahamu na pia tunaahidiwa ule urithi waliopewa wana wa Abrahamu pia.
Ndugu zangu, hii ndio faida ya kumwamini Kristo, ndio mshahara wenyewe. Paulo yeye alikuwa anaongea kutoka katika uzoefu wa maisha yake, yeye alikuwa amekwishaonja utamu, na faida yote ya kuwa chini ya Kristo, sasa alikuwa anawaalika wengine nao basi waje na kuzionja faida hizo.
Kweli ndugu zangu kuna faida kubwa sana kuwa chini ya Kristo; kutembea na Kristo maishani kuna utamu mkubwa sana. Tukiongozwa na Paulo leo, tuombe kutembea na Kristo.
Katika injili ya leo, tunaweza sasa kusikia habari za aliyeonja utamu wa Kristo: kweli Yesu alipokuwa anahubiri, mama huyu alipata habari njema na habari hii ilimfungua katika vifungo vyake na kuona raha kubwa sana. Kweli alimshukuru yule Mama aliyemleta Yesu duniani na kweli mama Maria alipata sifa kubwa sana hapa. Hapa ndugu zangu tujifunze umuhimu wa malezi kwa watoto wetu.
Mama Maria alipata heshima kwa namna Yesu alivyoishi; na yeye pia alimlelea vyema kabisa. Wazazi tukiwafundisha watoto wetu vyema, kweli ni faida yao kwani wanaheshimika. Wakiwafundisha watoto wao vibaya, wajue kwamba kila mtu atauliza, je, hawa ni wa wapi? Ni watoto wa nani? Mbona tabia zao ni mbaya sana? Na hapa ndipo wazazi wataaibika.
Kingine ndugu zangu ni kwamba nasi tukubali kuongozwa na wazazi na wakubwa wetu wanaotuongoza vyema. Tutambue kwamba tukikataa maongozi yao na kuishi vibaya, ni wao wanaaibika na kudharaulika, hivyo jamani tusiwaaibishe wazazi wetu, tubadilike, mzazi alikwisha tulea akatumia nguvu zake zote kutusomesha, kutulisha, wakatubeba mgongoni kwa miaka na miaka, wakatupigia vibarua, wakajinyima wakatusomesha-sasa jamani kwa nini tusiwapatie kipindi cha raha? Kipindi sasa wafurahie matunda ya watoto wao? Hizi tabia za kuishi ovyo zinawafanya wazazi wetu wafe katika huzuni.
Tubadilike-tuwafanye wazazi wetu wazeeke bila presha, jamani baadhi ya watoto kwa matendo yetu tunawaletea wazazi wetu presha, hii sio vizuri, tubadilike jamani. Mfanye mzazi afurahi kwa sisi kuwapo. Turudishe shukrani kwakuwajili pia. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni