Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Oktoba 09, 2020

Ijumaa, Oktoba 9, 2020,
Juma la 27 la Mwaka wa Kanisa

Gal 3:7-14
Zab 111:1-6 (K) 5
Lk. 11:15-26

ROZARI: TAFAKARI NA SALA ILIOJIKITA KATIKA KRISTO !

Karibuni ndugu zangu kwenye tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo basi katika tafakari ya neno Mungu, tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na mtume Paulo akiendelea kujibu hoja juu ya kukombolewa kwa njia ya imani. Anadai kwamba sote ni wadhambi na tunamhitaji Yesu Kristo atukomboe; hivyo anasisitiza kwamba imani kwa Kristo ni muhimu kuliko sheria au Torati ya Wayahudi. Hivyo wamtegemee Kristo, kKisto atawaokoa, waachane na kuweka matumaini yao kwenye sheria kwani sheria itawafanya watoke katika neema ya Kristo, wasitafute msaada toka kwa Kristo na kuhangaikia nguvu zao wenyewe na hapa wataishia kuanguka tu.

Hapa Paulo anamaanisha kwamba Kristo ndiye wa kutegemewa katika kila kitu; basi wamwelekee Kristo kwa kila kitu, wakipata shida yoyote wamwelekee, kabla ya kuanza chochote maishani mwao wamweleke Kristo kwanza. Kwa namna hii wataweza kufaulu katika mengi.

Hili ndilo tunaloalikwa kujifunza kwa siku ya leo. Kristo ni wa kutumainiwa kwa kila jambo; lazima kuanza na Kristo kwa kila jambo, kwa kila tunalofanya anza naye; kwa namna hii tutaweza kufaulu zaidi.

Katika somo la injili, tunakutana na Wafarisayo wakiwa wanazidisha chuki zao kwa Yesu, wanadai ati Yesu anatoa pepo kwa kutumia Beelzebul. Kweli hawa walikuwa na visa juu ya Yesu; Yesu alikuwa anatenda mema; hawaoni ahueni aliyowaletea wazazi, ndugu na huyu mgonjwa mwenyewe. Kweli wivu na chuki utatufanya tushindwe kuona hata wema wa mtu na uzuri wawenzetu na hapa tutakuwa tumewakatili sana watu. Chuki na wivu vitatukosesha mbingu na wengi wamekwisha umizwa kwa sababu ya chuki na wivu ndugu zangu.

Tubadilike, tuangalie ni kwa namna gani chuki zangu zimekwishanifanya nishindwe kuwafikia wenzangu.

Kingine watu wenye chuki na wivu wanarudisha maendeleo ya jamii nyuma. Ndugu zangu ni lazima kuondoa chuki na kukubali kwamba maishani kuna watu wanaokuzidi, wenye uwezo kukushinda na hivyo basi ni lazima ujifunze kuwapokea na kuungana nao. Fikiria kama wale viongozi wa Kiyahudi wangeungana na Yesu, unaonaje jinsi ile jamii ingekuwa tajiri? Ni wangapi wangaliweza kupona? Na maishani ni hivi hivi-kuna mahali unafika unaona kwamba kweli kama hawa ndugu au jamii ingeungana na kuwa kimoja, kama watu hawa na hawa wangaliondoa chuki na kuungana kweli wangalikuwa mbali zaidi.

Sisi tuache chuki, ni adui wa maendeleo kiroho na kimwili.
Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni