Alhamisi, Oktoba 08, 2020
Alhamisi, Oktoba 8, 2020,
Juma la 27 la Mwaka wa Kanisa
Gal 3: 1-5;
Lk 1: 69-75;
Lk 11: 5-13
KUOMBA!
Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo basi tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza; hapa tunakutana na Wagalatia wakikoromewa na Paulo. Hii ni kwa sababu wanamkosea Mungu adabu na kukosa shukrani. Wao walianzavizuri; walikuwa watu wa imani sana, na kweli waliweza kubarikiwa sana na Mungu kwa ile imani waliyoonyesha mwanzoni. Mungu aliwajalia neema nyingi sana. Lakini basi ilifika mahali wakasahau, wakaanza kufikiri kwamba neema walizozipata zilitokana na nguvu zao wenyewe; juhudi zao kwenye kushika sheria ya Musa.
Paulo anawaambia ni kwa imani. Isingekuwa imani-nguvu zenu zisingewafikisha popote. Anachosema Paulo ni cha muhimu na kwetu pia. Wapo wengi wetu unakuta mwanzoni tupo watu wa sala na kweli tunafanikiwa lakini baada ya mafanikio, tunamsahau Mungu, tunamtupa kana kwamba kile tunachofurahia tumekipata kwa nguvu zetu tu.
Mfano, kabla ya mitihani, tunakuwa tayari kusali sala zote lakini baada ya matokeo kutoka na kufaulu, Mungu hakumbukwi. Hili ni angalizo na kwetu hasa sisi tuliofanikiwa-yabidi kujiangalia ni kwa namna gani ninamtupa Mungu pembeni. Ninapokataa kusali rozari hasa kwa kipindi hiki, ni kumsahau Mama Maria ambaye kila wakati wa shida huja mbele yetu. Tunajivuna kwamba kwa nguvu zetu ndio tumeweza kuwa tulivyo. Tuache kumhuzunisha Mungu kiasi hiki. Kila mmoja aone huruma kwa dhambi zake jamani.
Katika injili tunakutana na Yesu akituambia kwamba tusali tukiomba. Ni kweli, kuomba kwahitaji subira na unyenyekevu mkubwa. Lazima tujifunze kwenda mbele ya Mungu tukiwa na subira na unyenyekevu. Tumwambie pia Mungu atimize matakwa yake.
Wengi wetu tunakosa subira. Tunataka tukiomba dakika hii tupate saa hiyo hiyo; halafu tunakosa tena unyenyekevu-tukienda kwa Mungu tunataka kumpangia anachopaswa kutupa. Tuwe kama akina Mama Teresa au Mt. fransisko wa Asizi. Kweli hawakumpangia Mungu cha kuwapatia, waliacha mapenzi ya Mungu yatimizwe ndani yao.
Nasi tuwe na utayari wa kukubali matakwa ya Mungu yatimizwe ndani yetu. Na tukienda mbele ya Mungu kuomba ni lazima tuwe na uvumilivu; kwa uvumilivu wetu tutayaokoa maisha yetu. Wengi wameyaangamiza maisha yao kwa kukosa uvumilivu. Wengi tumekosa mengi kwa kukosa pia uvumilivu. Tuokoe nafsi na maisha yetu kwa kuwa na subira.
Maoni
Ingia utoe maoni