Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Oktoba 06, 2020

Jumanne, Oktoba 6, 2020,
Juma la 27 la Mwaka wa Kanisa

Gal 1:13-24;
Zab 139: 1-3, 13-15;
Lk 10: 38-42.



KUMWELEKEA YESU!

Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana naomba nianze tafakari yake kwa kuuangalia wimbo wetu wa katikati. Hapa tunakutana na Zaburi ya 139 inayozungumzia juu ya Mungu kuujua na kuuchunguza moyo na akili ya mwanadamu. Mzaburi anakiri kwamba Mungu anajua kila kitu chake. Hivyo basi anakuwa mnyenyekevu na ombi lake kwa Mungu ili kwamba Mungu amsaidie ili basi amuongoze na kubakia kwenye njia njema, njia ya uzima.

Zaburi hii inatumika kutilia mkazo ujumbe wa somo la kwanza ambapo tunakutana na Paulo akijieleza waziwazi namna yake alivyo yeye na alivyopata utume wake. Anakiri kwamba utume wake asili yake ni Mungu mwenyewe, anasema dhambi zake zote alizowahi kufanya tangu ya kuwa mfuasi-anafanya hivi kwa sababu anajua kwamba Mungu anajua kila kitu chake na moyo wake na hakuna haja ati ya kujipaka mafuta na kujifagilia kwa maneno ya uongo mbele ya Wagalatia. Anakiri tena na kuwaambia kwamba neema ya Mungu ndiyo iliyomfanya hivyo na alishirikiana na mitume wa Yerusalem katika kuchukua majukumu yake kama mtu wa mataifa. Na anajionyesha jinsi alivyoweza kufanya bidii na kupokea vyema huu utume mpya aliopewa na Bwana.

Paulo ni fundisho kwetu ndugu. Mara nyingi sisi tunatabia ya kuficha mambo, tunataka tuelezee historia zetu nzuri tu mbele za watu ili tusilaumiwe au kuonekana wema. Lakini tutambue kwamba Mungu anajua moyo wetu wote. Na unapokuwa na ujasiri wa kuelezea hata makosa yako ya zamani, ni alama kwamba wewe unakiri kwamba ni neema ya Mungu iliyokuwezesha kufanya kazi ndani yako ikakubadilisha na hivyo basi unatoa ushuhuda na kumpatia Mungu utukufu. Unapoelezea historia yako ya uongofu kana kwamba tangu mwanzo ulikuwa mtoto mwema wa Kristo, mara nyingi ni kumdanganya Mungu na kumwonyesha kwamba tangu mwanzo ulikuwa na uwezo wa kufanya kazi bila uwezo toka kwa Mungu. Mungu ajua yetu yote. Tuwe kama Paulo. Tueleze historia zetu vyema.

Kwenye somo la injili tunakutana na Yesu akimueleza Martha kwamba Maria amechagua fungu lililobora. Yesu hapa hamlaumu Martha bali anamtaka afanye "balancing" na "moderation" ya mambo, ajue kwamba japokuwa kutumikia ni vyema, ni lazima mtu kujipatia muda wa kukaa chini ya Yesu na kumsikiliza. Tunafanya hivi kwa kufanya sala na tafakari.

Tujue kwamba maishani kuna sehemu ya Bwana. Tumwachie Bwana sehemu yake. Zaidi ni kwamba lazima pia baada ya kukaa chini ya Yesu na kumsikiliza, lazima kutoka na kwenda kutumikia. Sote ni mitume na wamisionari. Lazima uonyeshe utume wake kama mkristo kwa kutoka na kutumikia. Tusiwe wachoyo wa kukaa na Yesu na kusahau kutoka nje na kufuata shida za wengine. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni