Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Oktoba 07, 2020

Jumatano, Oktoba 7, 2020,
Juma la 27 la Mwaka wa Kanisa

Gal 2: 1-2, 7-14;
Zab 116: 1-2;
Lk 11: 1-4



NAMNA YA KUSALI

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi neno la Bwana katika somo la kwanza tunakutana na Paulo akijieleza mbele ya Wagalatia kwamba utume wake ni halali; anaendelea kujitetea dhidi ya wale waliofikiri kwamba yeye si mtume halali kama walivyokuwa akina Petro. Anajibu majibu ya wale waliofikiri tena kwamba utume wake alijitakia na hakuwa na muungano na mitume wengine. Yeye anajibu kiufahasa kabisa kuonesha kwamba utume wake aliupata kwa Yesu na yuko katika muungano na mitume wengine; yeye anasema kwamba alikubaliana na mitume wengine wote, anaonyesha muungano huu kwa kukubali hata kupeleka mchango kwa ajili ya kanisa la Yerusalem.

Paulo anajionyesha kwamba yeye ni mtii licha ya kwamba ni mtu mkali. Utii wa Paulo ulimwezesha Paulo kuhubiri ukristo kwa watu wa mataifa bila kuleta mtafaruku na mitume wengine. Angalikosa utii basi wale wakristo wake wangalikosa muungano na mitume wengine na kanisa lingalipasuka. Sisi wakristo hasa tulioviongozi wa dini tunaombwa tujifunze toka kwa Paulo. Hatuwezi kusonga mbele bila utii kwa kanisa na uongozi mzima, bila utii kwa Kristo. Tuache kujivuna, kazi ya kanisa ni kazi ya wengi, nisiifanye kwa maslahi yangu mwenyewe, lazima pia niwafundishe wakristo wawatii viongozi wote wa kanisa. Kuna baadhi ya vingozi tunawatenga wakristo, tunasema wawaheshimu viongozi hawa na kuwaheshimu hawa. Hii sio sahihi. Lazima tuwaheshimu viongozi wote waliowekwa na Mungu. Hapa tunaliletea kanisa letu maendeleo makubwa.

Kwenye somo la injili tunakutana na Yesu akifundisha sala ya baba yetu. Hapa anaanza kwa kuonyesha kwamba mwanadamu yupo ili amjue na amtukuze Mungu. Hili ndilo lengo la kwanza la uwepo wa Mwanadamu. Na pia asaidie kueneza ufalme wa Mungu.

Hapa twajifunza makubwa-ni lazima tujiulize, je, maisha yangu yanamtukuza Mungu? Kweli uwepo wangu umesaidia kumtukuza Mungu na kueneza ufalme wake? Tuangalie sana isije ikawa kwamba tunaeneza utawala wa shetani; tunapotuma mapicha machafu, au message chafu au kuongea maneno machafu tangu asubuhi hadi jioni bila kuongea ya Mungu, hapa tunaueneza utawala wa shetani. Lazima tufanya uwiano-yale ninayoongea, kuandika na kusikiliza-ni yapi mengi kuhusiana na Mungu-ni yale ya shetani au ya Mungu? Tueneze utawala wa Mungu.

Maoni


Ingia utoe maoni