Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Oktoba 05, 2020

Jumatatu, Oktoba 5, 2020,
Juma la 27 la mwaka wa Kanisa

Gal 1: 6-12
Zab 111: 1-2, 7-10
Lk 10: 27-37

“KATIKA JIONI YA MAISHA YAKO UTACHUNGUZWA TU JUU YA UPENDO” (Mt. Yohane wa Msalaba)

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi neno la Bwana tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na Paulo akiwakaripia wakristo wa Galatia. Hawa walikubali kufundishwa mafundisho mengine yaliyo kinyume cha injili-mafundisho haya yaliacha kutumainia Kristo, yaliiacha nguvu ya imani, yakaanza kuona nguvu ya juhudi binafsi zinavyosaidia katika utoaji wa ukombozi-ukombozi unaopatikana kwa kuishika sheria kama za vyakula, na usafi. Waliona kwamba Kristo hatoshi katika ukombozi-hawezi kuwapatia ukombozi bila ya wao kufuata sheria kama hizi. Huu ni ukosefu mkubwa wa imani kwa Kristo na ndio maana anaukemea.

Bado tunamhitaji Paulo atusaidie kukemea baadhi ya matendo yetu yanayomfanya Kristo aonekane kama hatoshi katika ukombozi. Tabia za ushirikina, kuvaa hirizi na kupiga bao na kufanya matambiko ni baadhi ya matendo yanayoashiria kwamba Kristo hatoshi kwenye kutupatia wokovu. Ukosefu wa imani umetufanya tushindwe kufaidi neema za Kristo, na kushindwa kutumika na Kristo kama vyombo vyake na kutumia gharama kubwa kuwanufaisha baadhi ya waganga. Pia vimetufanya tushindwe kuishi katika amani na wenzetu. Haya yanaharibu ukristo wetu kama wale wakristo wa Galatia. Tuache tabia za ukosefu wa imani namna hii.

Yesu katika injili ya leo anadhihirisha kwamba kuwa jirani wa mtu si hadi utokee naye eneo moja au kabila au taifa moja. Ujirani ni zaidi ya eneo; kila mmoja aweza kuwa jirani wa mwenzake. Basi tuwe majirani wa kila mmoja hasa sisi tunaoishi sehemu zenye mchanganyiko wa makabila na mataifa. Sio vizuri tukashikamana na watu wa kabila au ukoo mmoja tu na kusaidiana na kuwatenga watu wa makabila mengine. Ukristo ni zaidi ya kabila, ukoo au lugha au taifa. Tusaidie katika misiba, arusi na matibabu ya kila mtu bila ya kuangalia kabila au taifa au ukoo wake. Vikundi vyetu mbalimbali vinavyowaunganisha watu wa ukoo au kabila moja visitufanye tuache kuwasaidia watu wa makabila au koo nyingine. Tupendane ndani ya Kristo.
Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni