Alhamisi, Oktoba 01, 2020
Alhamisi, Oktoba 1, 2020.
Juma la 26 la Mwaka
Kumbukumbu ya Mt. Teresia wa Mtoto Yesu
Ayu 19: 21-27;
Zab 27:7-9.13-14;
Lk 10: 1-12
UFUASI MAANA YAKE UTUME
Ndugu zangu katika Kristo karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Tafakari yetu basi ya neno la Mungu, Ayubu anaendelea kuonesha imani ya hali ya juu kwa Mungu. Licha ya magumu yote yaliompata na dhoruba zote yeye anashuhudia kwa marafiki zake kwamba bado ana amini kwamba Mtetezi wake yaani Mungu yupo hai. Hataki kumkosea kabisa hata japokuwa ngozi ya mwili wake imeharibika. Anatamani uvumilivu wake na imani yake aliyo onesha kwa Mungu iandikwe kwa kalamu ya chuma ili watu wajifunze jinsi ya kumtumainia Mungu katika taabu. Na ama kweli Mungu ameyaruhusu yaandikwe na hadi sasa yanatutia moyo.
Ayubu anaonesha kwamba cha muhimu sio mwili wake wa sasa ulioharibika kwani anatambua atamuona Mungu pasipo mwili wake. Hili ni somo kubwa sana kwetu. Wengi wetu tumepoteza muda wote kushughulikia mwili tuu na tumezisahau roho zetu. Tumesongwa mno na kila tunachofanya ni kwa ajili ya mwili na hatukazani tena na roho. Kujiremba na kutengeneza mwili kumechukua muda mwingi kweli ukilinganisha na muda tuupatao wa sala. Tumehangaika kutafuta aina ya marashi, mafuta, sabuni,nk, lakini hatuhangaiki kutafuta padre wa kutuungamisha pale tutendapo dhambi. Tunakaa na dhambi mpaka tunafanana nazo.
Katika somo la Injili Yesu anawatuma wafuasi wake. Angalisho la Yesu kwa wafuasi wake ni kuacha yale ambayo yatatufanya tushindwe kutenda yale ya Mungu. Kuacha mkoba maana yake tusiwe na kitu chochote cha kutuchelewesha katika kutenda kazi ya Mungu. Mahangaiko na kuhangaikia mwili mno ni chanzo cha kushindwa kuwa wafuasi wazuri wa kushuhudia imani yetu.
Wafuasi wanaelezwa kwamba watende kazi na wanahakikishiwa uwepo wa watu wakuwakaribisha na kuwalisha. Hapa Yesu anawaonya kwa namna nyingine kuhusu kutafuta maslahi kwenye mambo ya Mungu-hiki huwa chanzo cha maporomoko ya utume. Tenda kazi ya Mungu, daima atakulisha tuu, kuanza kutafuta maslahi hufanya kazi hii isiendelee kabisa na badala yake, utume hufanyika tuu pale unapoona kuna faida binafsi. Tumuombe Mungu atusaidie kutenda kazi yake kwasababu sisi ni wafuasi wake na kwamba tunataka tumpelekee yeye mavuno ya roho za watu na sio mavuno ya vitu tulivyovuna kutoka kwa watu. Kila mmoja wetu ni mfuasi wa Kristo mletee Bwana mavuno yako kwa maisha yako mema.
Mt. Fransisko wa Asizi yeye hakutafuta mali wala kufungamana na mambo yakumshinda kumshuhudia Kristo na ndio maana alifanikiwa sana, leo ikiwa ni kumbukumbu yake tuombe neema ya kumuishi Yesu kama Fransisko alivyofanya kwa kujitoa kuishi maisha ya udogo kabisa na kumtumikia Yesu kwa unyenyekevu wa hali ya juu. Tumuombe Mungu atupe fadhila hii. Tumsifu Yesu Kristo
Maoni
Ingia utoe maoni