Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Oktoba 02, 2020

Ijumaa, Oktoba 2, 2020.
Juma la 26 la Mwaka

Kumbukumbu ya Malaika Walinzi

Kut 23: 20-23;
Zab 90: 1-6, 10-11;
Mt 18: 1-5, 10

MALAIKA –ULINZI WA MUNGU KWETU

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi tunaadhimisha kumbukumbu kwa ajili ya malaika walinzi; malaika wanaotembea nasi wakitulinda kila wakati. Uwepo wa malaika huyu ni alama kubwa sana ya upendo inayodhihirisha kwamba kweli Mungu anatupenda sana; katuwekea malaika anayeangalia kila hatua tunayofanya. Hili linapaswa kutufurahisha.

Lakini cha ajabu ni kwamba hili limewakasirisha wengi, wengi tumeona kana kwamba uwepo wa huyu malaika kama ati Mungu anazidisha kutufuatilia, hatupatii uhuru, hivyo basi wengi wetu tumemfukuza-na huyu malaika akishakaa pembeni, huo ndio mwanzo wa maanguko wa maisha ya mwanadamu kwani yeye hubakia bila mlinzi na shetani hutukamata kirahisi. Huyu ndiye malaika mlinzi.

Masomo yetu leo tena yanatukaribisha vyema kwenye kuuona ukuu wa malaika huyu. Mzaburi katika wimbo wa katikati anatueleza jinsi Mungu alivyomuweka huyu malaika akielewa kila tunachofanya, na jinsi Mungu asivyopenda njia yetu hata moja ishindwe kutuongoza mbele kwa Mungu.

Somo la kwanza linatuonesha jinsi Mungu alivyowapatia malaika wa namna hii wana wa Israeli walipokuwa kule jangwani ili awawezeshe kupita ndani ya lile jangwa. Lile jangwa lilikuwa ni jangwa baya sana. Lilijaa nyoka wa sumu, makabila yenye hasira, na ukame mwingi sana. Hivyo walihitaji wa kuwaongoza ili wawaepe hawa maadui na kweli malaika mlinzi alifanya kazi hii vyema. Pale waliposhirikiana na huyu malaika, kweli walifaulu, walipata chakula, hawakushambuliwa na kabila lolote na hakuna nyoka aliyewadhuru.
Lakini walipoonesha ukaidi, walijikuta wakikumbana na nyoka tena wenye sumu, makabila yenye hasira, na ukame wa hali ya juu na kiu.

Yesu katika Injili anatuambia kwamba bado tunaye malaika wa namna hii kwa kila mmoja. Hivyo tumtegemee huyu malaika. Tumwalike, atuepushe na nyoka wa sumu wa hapa dunia, atuoneshe tukanyage wapi, atuepushe na ajali mbalimbali. Bila huyu malaika tutadumbukia kwenye mitego mingi sana ya shetani ya ulimwengu.

Wengi tumedumbukia kwenye mitego ya uasherati, hasira, ulevi na tamaa kwa sababu ya kumtupa pembeni huyu malaika. Na kubakia bila mlinzi-hii ni hatari sana-kubakia bila mlinzi.
Tusikubali kubakia bila huyu malaika kwani kwa hakika tutapeperushwa kirahisi na shetani.

Kingine tutambue kama injili inavyotueleza kwa siku ya leo kwamba tusimuonee yeyote aliyemdogo kwa sababu ya uwepo wa malaika wanaowalinda watu kama hawa. Waweza kutumia nguvu nyingi kutaka kudhulumu aliyemdogo lakini bado tukashindwa. Yeye akianguka magotini kwa Bwana na kupata ulinzi wa huyu malaika, hakika hutamshinda. Na zaidi tutapata laana. Tusiwaonee wadogo ili tusije tukapata laana za kuadhibiwa na huyu malaika.

Pia tushirikiane naye kama Mwenyezi Mungu anavyowaeleza wana wa Israeli leo. Wengi tunakosa ushirika naye na ndio maana tunaanguka kirahisi katika mitego ya shetani. Na pale tunapotenda dhambi, huwa tunamkufuru kwani yeye yupo na dhambi zetu zinasababisha ukuta kati yetu na yeye. Tukimbie dhambi ndugu ili malaika wetu awe karibu nasi zaidi. Tumsifu Yesu Kristo

Maoni


Ingia utoe maoni