Jumatano, Septemba 30, 2020
Jumatano, Septemba 30, 2020,
Juma la 26 la Mwaka wa Kanisa
Ayu 9: 1-12, 14-16
Zab 87: 10-15
Lk 9: 57-62
GHARAMA YA KUWA MFUASI WA KWELI WA KRISTO!
Karibuni tena kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi tafakari yetu inaanza kwa kuliangalia somo la kwanza toka katika kitabu cha Ayubu. Hapa tunakutana na Ayubu akiwajibu wenzake kwa hekima kubwa; anasema hata kama mimi naonekana kana kwamba nimeonewa, Mungu bado anabakia kuwa hakimu bora na mwenye haki. Anatambua kwamba uwepo wake ni upendeleo toka kwa Mungu-tena anatambua zaidi kwamba Mungu ameumba makubwa zaidi kuliko hata yeye (Ayubu). Yeye ni sehemu ndogo tu ya uumbaji wa Mungu. Akitambua hilo basi, anaona kwamba kilichobakia ni yeye tu kumlilia Mungu-kama inavyoelekezwa kwenye zaburi yetu ya wimbo wa katikati na hakika Mungu hatamuacha.
Moyo huu wa matumaini na unyenyekevu ndio unaopaswa kutuingia na sisi ndugu zangu. Itatokea kipindi ambacho hata sisi tutaingiwa na magumu kama yaliyompata Ayubu. Wakati huu sio wakati mrahisi-ni wakati wa kumweleza Mungu kwamba “Ee Mungu tayari umefanya makubwa, umeumba dunia yote hii, umeumba milima mikubwa kabisa, umetupatia pia binadamu wenye uwezo na maarifa makubwa kabisa. Ninakushukuru kwa kuniumba na mimi pia. Ninakuomba hakika usiniache ee Mungu-nisaidie katika shida yangu. Hakika Mungu ataonesha upendo wake mkuu.
Wengi wetu tumetumia kipindi cha magumu kama kipindi cha kukata tamaa. Kinatakiwa kitujenge na mwishowe tuvune mazao ya kipindi hiki kwa kutufanya tuwe watu wa imani zaidi. Leo tujichunguze na kujiuliza, je, vipindi vya mateso vimetuongezea imani?
Kwenye somo letu la Injili leo tunakutana na watu mbalimbali wanahusishwa na safari ya kutaka kumfuata Yesu. Wa kwanza anakuja kwa Yesu na kuahidi kumfuata kila atakakokwenda-huu ni utume mgumu sana kwani ni wachache tu walioweza kumfuata Yesu kila alikokwenda. Hata mitume wake wengi walikimbia ilipofikia ile saa ya mateso. Hivyo basi huyu aliongea kwa hisia bila kutambua gharama ya wito kumfuata Yesu.
Wa pili anachaguliwa na Yesu kabisa tofauti na yule wa kwanza na kualikwa kumfuata Yesu. Yesu anamuona kuwa na uwezo wote na nguvu zote za kuweza kumfuata. Lakini basi anamwambia Yesu asubiri kwanza na atamfuata baadaye. Hili ni jibu la walio wengi hasa nyakati zetu tuikaribiapo Ekaristi. Yesu anajitokeza akitualika kila siku tumpokee kwenye Ekaristi, lakini basi sisi kutokana na uchumba wetu sugu au dhambi zetu, tunamweleza kwamba asubiri kidogo kwanza hadi tufanye dhambi na tukishachoka ndio tutamfuata tukiwa wazee. Au tunamueleza kwamba tutakufuata lakini subiri kidogo hadi tutende dhambi zaidi na tukishakuwa wazee ndio tutakufuata.
Hili ndio jibu la walio wengi kati yetu. Yesu anataka tuoneshe nia na kuitikia kwa kusema kwamba Ee Mungu niko tayari kukufuata na kumfuata Yesu ni sasa, kushiriki Ekaristi ni sasa, tusitegemee muujiza uzeeni kwamba tutaanza kuwa wema zaidi. Tuanze kuwa wema tangu sasa. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni