Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Septemba 28, 2020

Jumatatu, Spetemba 28, 2020,
Juma la 26 la Mwaka wa Kanisa


Ayu 1:6-22
Zab 17:1-3.6-7
Lk 9: 46-50

KUJITEGEMEZA KWA MUNGU BABA YETU!
Karibuni ndugu zangu kwenye adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu inaongozwa na zaburi ya wimbo wa katikati “Ee Bwana utegee sikio lako usikie sala yangu”. Haya ni maneno ya Mzaburi akimlilia Mungu baada ya kupata shida nakumweleza tazama wewe ndiwe kimbilio langu sina mwingine. Tazama nimepatwa na shida na wewe ndiwe wakunisaidia.

Zaburi hii imetumika kutilia mkazo ujumbe wa somo la kwanza ambaye anayekumbwa na shida nyingi hivi ni Ayubu kwakweli anakumbwa na misiba. Watoto wake, wanyama wake ambao ndio utajiri wake unateketea na anabaki bila msaada wowote. Yeye basi hakati tamaa anapeleka mateso yake yote kwa Mungu. Anamweleza Mungu asimwache aje upande wake, yeye ndiye aliye muumba asikubali ashindwe na haya matatizo.

Moyo huu wa Ayubu ndiyo moyo unaohitajika kwetu sisi wakristo, kweli tupo ambao tunakumbwa na shinda nyingi sana na ugumu mkali kabisa. Tunapigika sana lakini niwachache tunaokuwa na moyo wa ulivu kama huyu Ayubu, ni wachache tunaomkimbilia Mungu kwa mara moja kama alivyofanya Ayubu. Tunapaswa kujikabidhi mikononi mwa Mungu pindi shida itokeapo. Huu ni ujumbe ambao tunapaswa kuupeleka kwa wote tunaokutana nao leo hasa wale wanaoteseka. Na ukweli ni kwamba ni wachache kati yetu wenye Imani ya namna hii, ya kuwa na Imani ya kwamba Bwana ndiye wakusaidia. Tuwaeleze kwamba Bwana atasaidia endapo watapeleka shida zao kwake, tuwaombee pia wale wanaoteseka na kuwaonesha kwamba tumaini lao kuu ni Mungu.

Katika somo la Injili tunakutana na Yesu akikemea mabishano kati ya wanafunzi wake kuhusu ni nani aliye mkubwa miongoni mwao. Yesu anawaeleza kwamba aliye mkubwa ni yule aliye mtumishi wa wote. Na hili ni kweli ndugu zangu. Unyenyekevu huja kabla ya heshima. Unyenyekevu ndio ukupatiao ukuu, ukuu hauji kwakulazimisha bala kwa taratibu tuu, ukweli ni kwamba ukuu hauutangazi mwenyewe bali ukuu wako hutangazwa na wengine.

Wakina Mt. Fransisko wa Asizi waliupata ukuu kwa unyenyekevu wao na kuwa mtumishi. Pale mahali ambapo familia au jumuiya inapo nyenyekea mambo yake huwa safi-lakini ikishaonesha majivuno tuu, ndio mwisho wao tena huanza kuporomoka. Kila mmoja basi tutambue ubaya wa majivuno. Majivuno yameangusha wengi sana na jamii kwa ujumla. Lakini unyenyekevu umekuza wengi sana. Basi tuone thamani ya unyenyekevu kwa kila mmoja wetu. Tuachanae na majivuno ambayo yamewaangusha wengi sana. Sisi tusiige mifano yao tusije kuangushwa.
Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni