Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Septemba 25, 2020

Ijumaa, Septemba 25, 2020,
Juma la 25 la Mwaka wa Kanisa

Muh 3: 1-11
Zab 143: 1-4
Lk 9: 18-22

KRISTO NI NANI KWANGU?

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza na hapa tunakutana na tafakari saafi kabisa. Tunaambiwa kuna wakati maalumu kwa kila kitu. Upo wakati huu. Kuna wakati wa kulia na kuomboleza, wakati wa kukusanya na kutapanya,wakati wa kukaa kimya na wakati wa kuongea. Kweli hii ni tafakari alioifanya mtu mwenye hekima na akaona ili mwanadamu aweze kufanikiwa, ni lazima awe na hekima ya kuwa na kiasi, ni kama Mwanafalsafa Aristotle alivyosema kwamba “mwenye hekima ni yule ambaye anaweza kutambua “balance” ipo wapi.”

Hiki ndicho tunachokosea. Magomvi mengi na makosa mengi hutokea kwasababu hatujui kusoma mazingira, mazingira ni muhimu sana, yakutufundisha jinsi ya kuepuka magomvi mbali mbali maishani. Wengi wetu tunapotea pale tunaposhindwa kutambua kwamba kuna muda fulani ambao tunapaswa kufanya biashara na muda fulani wa kukaa chini ili kusali kwa Mungu. Wengi tunatumia muda wote kwenye kufanya kazi. Kuna muda wa kusali na kufanya kazi. Tumuombe Mungu hekima ya kutumia kila kitu kwa hekima, tuwe na kiasi, tujue kila kitu lazima tuwe na kiasi, tunapo ona chupa za bia mbele yetu tukumbuke kuwa na kiasi, familia nyingi zimekosa Amani kwasababu ya ulevi. Ukosefu wa kiasi umewaangusha wengi sana. Tukiwa na kiasi tutakuwa na hekima ya kutumia vya dunia vyema.

Kwenye somo la Injili, Yesu anawauliza wanafunzi wake ya kwamba watu wanasema yeye ni nani? Wanafunzi wanasema Yohane Mbatizaji, wengine Elia na wengine moja wapo wa manabii wa kale. Lakini Yesu aliwataka na wao watoe majibu na Petro akajibu kwamba Yesu ni Masiha. Sisi lazima tuwe kama Petro. Patro alimtafakari Yesu alikutana na Yesu na upendo wake maisha mwake.

Na sisi ndugu zangu kila mmoja wetu ni lazima aweze kujibu Yesu ni nani maishani mwake? Lazima tuweze kumjibu kwamba wewe ni Masiha-kwamba mpaka sasa umeweza kuyakomboa maisha yangu yote na hivyo Ee Yesu wewe kwangu ni Masiha. Njoo uyatawale maisha yangu, tawala familia yangu nijalie hekima kama ya Muhubiri katika somo la kwanza niweze kutambua ya kwamba kila jambo lina wakati wake. Tamaa ni adui mkubwa, anayetufanya tushindwe kutambua kwamba kila jambo lina wakati wake. Tunakuomba uziongoze na kuzipa adabu tamaa zetu. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni