Jumanne, Septemba 22, 2020
Jumanne, Septemba 22, 2020
Juma la 25 la Mwaka wa Kanisa
Mit 21: 1-6,10-13
Zab 118: 1, 27, 30, 34-35, 44
Lk 8: 19-21
FAMILIA YA MUNGU!
Karibuni ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo katika somo la kwanza toka katika kitabu cha Mithali bado linazidi kutoa wosia juu ya faida zipatikanazo kwa kumcha Bwana Mungu wa Israeli. Kumtii Mwenyezi Mungu kutakuwezesha kukaa katika hema ya Bwana-haya ni maneno matamu kabisa ndugu zangu.
Na leo katika somo letu la kwanza, utii unapewa nafasi ya pekee-somo letu linasema kwamba kutii na kutenda yaliyo mema ni bora zaidi machoni pa Bwana kuliko dhabihu au sadaka yeyote ile. Utii humkweza mwanadamu, na kumfanya wa faida na msaada zaidi ulimwenguni. Kiburi kiliwaangusha wafalme maarufu; Mfalme Sauli alikosa utii na kupoteza ufalme wake, Mke wa Luthu alipoteza uhai wake kwa kukosa utii. Musa alipokosa utii kwenye maji ya Meribah, alinyimwa nafasi ya kuingia ndani ya nchi ya ahadi na kuifurahia baraka zake. Lakini utii uliwakweza wengi. Utii ulimkweza Abrahamu na kumfanya awe Baba wa taifa Teule; utii ulimkweza pia Daudi toka kuwa mchungaji na kuwa mfalme ndani ya taifa la Israeli. Sisi tuwe watii, tutakuwa wa faida zaidi na utii utatukweza.
Kila mmoja wetu huzaliwa akiwa mkuu tayari machoni pa Mwenyezi Mungu. Lakini kwa bahati mbaya wengi wetu tumeanguka na tuko maskini kwa sababu ya kiburi. Kiburi kimetuangusha sana na hadi leo tumeshindwa kupiga hatua. Tuwe na uvumiilivu nasi tutapiga hatua kubwa zaidi.
Kwenye somo la injili tunakutana na Yesu akisisitizia kwamba Ndugu zake ni wale walisikiao neno la Mungu na kulishika. Hawa huzaa sana. Kwenye injili ya Luka, Yesu anasema maneno haya baaada ya ule mfano wa mpanzi na mbegu ambapo alizungumzia makundi mbalimbali ya watu na namna walivyolipokea neno la Mungu. Kulisikia neno la Bwana na kulishika ndiko kutuwezeshako kuzaa matunda mema. Wengi wetu hatuzai matunda mema kwa sababu hatuko kabisa na Bwana.
Zaidi tena ni kwamba ukilisikia neno la Bwana na kulishika, ndiko chanzo cha wewe kuwa ndugu wa Yesu na kuwa ndugu wa kila mmoja. Kulishika neno la Yesu hutufanya sote tuwe ndugu. Udugu wetu ni mpana zaidi ya familia zetu, tunajiongezea idadi ya marafiki kwa kulishika neno la Bwana. Tusipolishika neno la Bwana, tunaongeza uadui kati yetu na wenzetu. Ukilishika neno la Bwana utakuwa na utayari wa kuishi mahali popote bila hofu. Kulishika neno la Bwana kuliwasaidia watu kama akina Abrahamu kuweza kuishi katika nchi ya kigeni, kuliwasaidia akina Daudi kupigana na maadui wakubwa kama akina Sauli na kuwashinda kwa sababu walishika sheria za Bwana. Sheria za Bwana humwongezea yeyote idadi kubwa ya Ndugu na ulinzi wa kuishi na yeyote. Tuishike sheria ya Bwana nasi tutakuwa salama zaidi.
Maoni
Ingia utoe maoni