Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Septemba 23, 2020

Jumatano, Septemba 23, 2020.
Juma la 25 la Mwaka

Mit. 30:5-9
Lk 9: 1-6


KUNGUTA MAVUMBI: NAKUACHA MAMBO YA ZAMANI

Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwenye tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo basi katika neno la Bwana somo la kwanza toka katika kitabu cha Mithali, tunakutana na mwandishi akiomba ombi nyofu mbele ya Mwenyezi Mungu: kwamba asimfanye tajiri sana ili basi asije akamsahau Mungu na kushindwa kuona ukuu wake au asimfanye maskini kiasi cha kuja kuwa mwizi.

Utajiri hutufanya tuzidishe majivuno na kuona kwamba Mungu hahitajiki; tunakosa hamu ya kusali, na kutokuona umuhimu wa kuanguka magotini kwa Mungu kunyenyekea. Hii ni kinyume na hali ya mwanadamu; mwanadamu ameumbwa kiumbe maskini mbele yake, ni lazima tuanguke kila siku magotini mwake. Tuwe makini na vijipesa vinavyotuongezea kiburi na kufikiri kwamba sisi tuna nguvu sana lakini hatuna kitu. Hatma ya mwanadamu kweli ni kuwa mnyenyekevu.

Halafu pia kwa upande mwingine, umaskini, hasa kwa aliyekosa moyo wa kuridhika hutufanya tuhangaike kila wakati tukitafuta chakula cha kujaza tumbo letu hata kwa wakati mwingine tunadiriki kuiba. Umaskini hutufanya tuibe hata muda wa sala, tunamwibia Mungu hata jumapili yake na kwenda kulima au hata kufanya biashara. Na hapa kwa wengi tumekamatwa tayari. Kweli tumekwishamuibia Mungu sana. Sisi nasi yawezekana tukawa watu wenye vipaji mbalimbali; lazima tuhakikishe kwamba vipaji hivi vinamletea Mungu sifa; mara nyingi vimekuwa sehemu ya Mungu kudharauliwa. Sisi tuvitumie kumpatia sifa.

Katika somo la injili, Yesu anawapatia wale 12 uwezo juu ya pepo wachafu wote. Sisi nasi tunapokea nguvu hizi kwa kuwa wafuasi wa Kristo hasa kwa njia ya sakramenti ya ubatizo. Sisi tutambue mamlaka yetu. Tumepewa mamlaka juu ya nyoka na nge wote wa ulimwengu huu. Tatizo letu ni kuogopa na kutokujiamini. Tambua uwezo ulionao. Acha kuwa mwoga na mvivu. Shetani anatushinda wengi kwa sababu ya woga wetu na uvivu. Tupambane na hivi viwili-woga na uvivu nasi tutamshinda shetani. Tusikubali shetani aendelee kututawala. Tumpinge kwa nguvu zetu zote

Maoni


Ingia utoe maoni