Jumamosi, Septemba 19, 2020
Jumamosi, Septemba 19, 2020,
Juma la 24 la Mwaka wa Kanisa
1 Kor 15: 35-37, 42-49
Zab 55: 10-14
Lk 8: 4-15
UFUFUKO: LENGO LA MAISHA YETU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi neno la Bwana linaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na Paulo akiendelea kujibu changamto zilizolikabili kanisa la Korintho na bado kwa leo anaendelea kujibu changamoto juu ya ufufuko wa wafu. Changamoto zilitolewa kwa sababu ya uwepo wa wanafalsafa wengi katika Korintho waliowakejeli wakristo kama watu wanaodanganyika kirahisi kama wangalikubali suala la ufufuko; na waliwapatia changamoto-waliwauliza kwamba sasa mtu akifufuka anachukua mwili gani kwani tunajua kwamba mwili wote huoza?
Sasa tunajua kwamba hakuna kitu kinachoweza kutoka katika utupu "something can not come from nothing": sasa inakuwaje mwili unaoharibika uzae mwili usioweza kuharibika na kudumu milele, yaani mwili wa umilele uzalishwe na mwili usiokuwa na umilele? Swali hili liliwatatanisha hadi wakristo na baadhi yao kwa kuziogopa zile falsafa, ilibidi watake majibu toka kwa Paulo. Paulo anawajibu leo kwa msisitizo mkubwa-anashangaa kuona kwamba wanaruhusu falsafa ziwanyime usingizi na kuitatanisha imani yao-anawaeleza kwamba mambo ya dunia ni tofauti na mbingu, Adamu wa kwanza alileta kifo lakini Yesu ambaye ni Adamu wa pili ameleta uzima kwani yeye ni wa mbinguni na Bwana wa uzima. Wakimtumainia hakika nao watapewa uzima.
Anayalinganisha maisha yajayo kama mbegu ambayo basi ili iweze kuota, lazima ife na mwili wake kuharibika ili iweze kuzalisha mwili mpya ulio na ubora zaidi. Sisi nasi ni kama mbengu-miili yetu nayo itasiwa ardhini-mwili utakaozalishwa toka hapo utategemea namna jinsi tulivyoishi imani yetu. Imani ni uhai ndani ya miili yetu dhaifu, kama dhahabu ndani ya vyombo vya udongo, iliyo na uwezo wa kuipatia thamani kuu miili yetu na kuipatia thamani ile siku ya mwisho. Sisi ni lazima tuwe watu wa imani, tutende matendo mema, na kufadhili. Haya yote yatatupatia thamani kubwa zaidi ile siku ya mwisho.
Katika injili Yesu anafananisha imani na mbegu ambayo hudondoshwa mioyoni mwa kila mmoja. Wengine mioyo yao ni mikavu kama miamba na hivyo imani hiyo hushindwa kutoa mizizi na wengine mioyo yao ni mizuri na tajiri kama udongo mzuri na udongo huu huwezesha imani hii kuzaaa. Wengi hatuipatii nafasi imani yetu kukua, kweli tunaisongasonga na shughuli nyingi za kidunia. Hakuna muda wa kusali, au tafakari kupalilia imani yetu. Tumekuwa wachoyo wa muda kwa ajili ya Mungu na kwa baadhi yetu simu zinakula muda wetu sana. Haya yote hayana nguvu ya kuweza kuifufua miiili yetu kwa ile siku ya mwisho. Haya yanaozesha.
Sala na tafakari na matendo ndiyo itakayoipatia miili yetu nguvu na thamani ya upya itakayotufufua. Tupanie kutenda mema. Tusiufinye muda wa sala sana, siku hizi muda huu unaonekana kama muda wa kifungoni, kwa wengi wetu bado hatujaweza kuufurahia muda huu. Tuufurahie muda huu zaidi na zaidi.
Tumsifu Yesu Kristo
Maoni
Ingia utoe maoni