Jumanne, Septemba 15, 2020
Jumanne, Septemba 15, 2020
Juma la 24 la Mwaka wa Kanisa
Kumbukumbu ya Bikira Maria Mtakatifu wa Mateso
Ebr 5: 7-9; au 1Kor 15:1-11
Zab 30: 2-6, 15-16, 20;
Yn 19: 25-27, 35 au Lk 2: 33-35
KUTESEKA KWA AMANI NA FURAHA!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi tunaadhimisha kumbukumbu ya Maria mama wa Mateso. Sherehe hii huadhimishwa tarehe 15 Septemba kila mwaka baaada ya tarehe 14 Septemba baada ya sherehe ya kutukuka kwa msalaba ambapo basi Yesu alikuwa amenyanyuliwa juu kabisa ya msalaba huu akipata mateso makubwa, Maria Mama yake alisimama karibu kabisa ya msalaba huu akiteseka moyoni mwake.
Mateso haya huonyeshwa kwa mfano wa Maria akiwa katika uchungu mkubwa, akimwagika machozi na mishale saba ikiuchoma moyo wake na kusababisha damu nyingi kuvuja. Chanzo chake ni utabiri alioutoa Simeoni kwamba wewe upanga uchakuchoma. Kiteologia ni kwamba Mama huyu alipatwa na mateso makuu saba: kwanza unabii wa Simeoni, pili kukimbia kwenda Misri, tatu ni kupotea kwa mtoto wake na baadaye kumkuta hekaluni, nne kukutana na mamaye kwenye njia ya Kalvario, halafu ni kumwona akisulibishwa msalabani Kalvario kuchomwa Yesu ubavuni kwa mkuki na baadaye kushushwa msalabani ambapo Mama Maria alimpokea na kumbeba mikononi, saba ni maziko ya Yesu.
Kwa matukio yote ya leo, ule unabii wa Simeoni kwamba wewe upanga utakuchoma kweli ulitimia maishani kwa huyu Mama. Mateso haya yalipokelewa na moyo wa uhodari, uliojaaa mapendo na ulioendana na jibu lake alilosema-mimi ni mtumishi wa Bwana, na nitendewe kama ulivyonena.
Sherehe hii iliingizwa rasmi katika misale ya kanisa mwaka 1482. Papa Pius wa kumi mnamo mwaka 1814 aliidhinishwa kumbukumbu hii ifanywe tarehe 15 Septemba kila mwaka. Sherehe hii huonyesha Maria kama mama wa Mkombozi, kweli aliteseka pamoja na mtoto wake katika ukombozi wa ulimwengu.
Lakini aliyapokea haya kwa upendo mkubwa na uchungu na ukomavu aliounesha Mama Maria wakati wa mateso ya mtoto wake na kweli aliweza kushiriki katika utukufu wake; hakukata tama.
Hili ni funzo kubwa la kujifunza kwetu. Kipindi cha mateso ni kipindi cha kumwomba Mungu atufundishe hekima kubwa ya kuyapokea ni kipindi ambacho wengi hupoteza imani. Kwenye jamii zetu, kipindi cha mateso makubwa huwa tunatabia ya kutafuta chanzo; tunamuuliza Mungu atupatie chanzo kwa haraka haraka na mwishowe basi tunaona kwamba Mungu hajatupatia chanzo, tunaingia kwenye ushirikina na kuuliza chanzo ni kipi? Na hapa tunapewa masharti ya ajabu na sisi huwa tunayatekeleza. Maria anatufundisha ukomavu wa kupita vipindi kama hivi. Lazima tuvifanye vipindi vya neema na kubarikiwa na Yesu zaidi na zaidi kama Maria alivyoweza kukifanya kuwa ni kipindi cha baraka kwake na si cha kukosa imani.
Kingine cha kujifunza ni yale tunayokutana nayo kwenye injili ya leo. Tunaambiwa kwamba Mama Maria alikuwa chini ya msalaba pamoja na Yesu akiyavumilia mateso pamoja naye hadi ile safari ya mwisho. Maria anakuwa funzo kwetu. Ukweli ni kwamba maishani kukutana na mtu atakayekuonesha upendo kama Maria kwa Yesu sio rahisi-atakayekuwa hadi mwisho wa safari sio rahisi. Au kukutana na mke atakayesafiri nawe hivi sio rahisi. Wengi tunachoka haraka sana tukishaaanza kusaidia watu. Utafikia mahali utaonekana kuwa kero.
Lakini Maria anatufundisha jambo kubwa leo. Kwamba ni lazima tuwe wafuasi waaaminfu, ingia na shiriki njia ya mateso ya mwenzako hadi mwisho. Usiishie njiani. Kama ni mume mgonjwa nenda naye hadi mwisho. Tuache kuwatelekeza na kuchoka kwa haraka.
Kuna shetani anatufundisha vibaya tutelekeze watu; tumtambue huyu shetani, analeta uvivu-pambana naye kabisa. Hata kama ni madaktari watambue hili-tusiwatelekeze wagonjwa kwa haraka na kwa urahisi.
Mama huyu anabakia kuwa mfariji wetu hasa kwa wanaoteseka. Anatuambia kwamba nami nilipitia mateso kama hayo. Yapokee, utashinda siku moja, mimi nipo kukutia moyo na kukuongoza.
Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni