Jumatano, Septemba 16, 2020
Jumatano, Septemba 16, 2020,
Juma la 24 la Mwaka
1 Kor 12:31 – 13:13;
Zab 32: 2-5, 12, 22;
Lk 7: 31-35.
KUFUNGUA MIOYO YETU KWA YESU
Karibuni tena ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Tukianza kwa kuliangalia somo la kwanza, bado tunakutana na mtume Paulo akiendelea kujibu changamoto zilizolikumba kanisa la Korintho. Changamoto anayokumbana nayo leo ambayo basi hata jana alikwisha anza kuitatua ni ile ya matumizi ya karama za bwana ndani ya kanisa huko Koritnho. Ni kwamba kanisa la Korintho lilibarikiwa sana hasa kwa upande wa karama.
Kulikuwa na walioweza kuponya, wengine wakawa manabii, wengine waliweza kunena kwa ndimi, na wengine waliweza hata kutafsiri kile kilichonenwa kwa ndimi. Lakini basi kilichotokea ni kwamba walionena kwa ndimi walijiona kuwa na karama bora zaidi kuliko wengine. Hivyo basi ilitokea kwamba hata baadhi ya waamini walianza kutamani kuwa na karama hii wakadharau karama nyingine.
Paulo anasema kwamba kanisa linazihitaji karama zote hizi nani lazima lijengwe nazo. Hivyo anasema kwamba waache kuona kushindana juu ya karama na iliyopo ni wao kuwa na upendo. Upendo ndio utakaowawezesha kulijenga kanisa la Mungu na kuwa na manufaaa zaidi.
Hii ni kweli ndugu zangu-upendo ni yote. Unakuta kwamba jamii ina uwezo kidogo lakini kwa sababu ina upendo na kushirikishana kile kidogo walichonacho, basi wanaweza kufanya mengi zaidi mno kuliko jamii ile yenye uwezo bila upendo. Hii ni kweli ndugu zangu na kila mtu ashuhudie. Penye upendo-kweli pana nguvu sana na hata kama mtu anapesa kiasi gani-kamwe hawezi kupambana na jamii iliyo na upendo na mshikamano akaishinda. Mkishakuwa na upendo kushindwa sio kirahisi.
Hivyo tuthamini upendo. Karama ikipaliliwa na upendo huzaa mengi. Wengi wameishia kupoteza akili zao bila kutumika, wengi wameishia kutokutumia chochote kwa sababu ati ya kukosa upendo-ukosefu wa upendo umefanya wengi wadumae lakini upendo umenyanyua wengi.
Tuwe basi na upendo. Kweli upendo ni wa faida sana kwa kanisa na kwetu pia.
Kwenye somo la injili Yesu anakishangaa kizazi hiki kwani kinachezewa ngoma, kinaambiwa kifanye jambo hili lakini basi hakifuati. Kina ukaidi mkubwa na ukosefu wa upendo na hivyo basi kimeshindwa kutambua na kusoma alama za ulimwengu. Hii yote ni kwa sababu kilikosa upendo na kuwa na majivuno. Kikaona watu kama akina Yohane Mbatizaji na Yesu kama vituko tu. Kilitaka mawazo na mipango yao ifuate hali ya kuachana na wengine.
Sisi tuachane na mawazo kama haya ya hiki kizazi kwa kuwa watu wenye upendo zaidi, mshikamano na kuacha majivuno. Majivuno yametufanya tusiwe wa faida ndani ya ulimwengu. Tumsifu Yesu
Maoni
Ingia utoe maoni