Alhamisi, Septemba 17, 2020
Alhamisi, Septemba 17, 2020,
Juma la 24 la Mwaka
1Kor 15:1-11
Zab 117: 1-2, 15-17, 28;
Lk7: 36-50.
KUOMBA HURUMA
Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu tena asubuhi ya leo. Bado tunaendelea kuongozwa na tafakari ya neno la Mungu toka katika kitabu cha waraka wa kwanza wa mtume Paulo kwa Wakorintho. Na bado anaendelea kujibu maswali na changamoto zilizoikumba ile jumuiya. Na leo anazungumzia changamoto juu ya suala la ufufuko. Wakristo wa Korintho waliishi kati ya wanafalsafa waliowakejeli juu ya suala la ufufuko baada ya wafu. Walikuwako wanafalsafa kama akina Epicureans waliosisitizia juu ya kuponda mali na anasa. Wakati huu falsafa hii ilikuwa imeshika kasi sana na hawakuamini ufufuko.
Wakristo walimtegemea Kristo aje kwa haraka ili basi awafufue wale wakristo waliokuwa wakifariki kabla ya Kristo kuja ili basi wale wanafalsafa wapate kuoneshwa kwamba walichokifundisha sio sahihi. Lakini basi Yesu hakufika kwa haraka vile walivyokuwa wakihisi na hivyo basi wakauliza je, kwa nini? Wanafalsafa hawa waliwakejeli sana wakristo na imani yao juu ya ufufuko kwa kuwaambia kwamba ni uzushi.
Lakini basi Paulo anajibu suala hili na kwa kuanza kusema kwamba kwanza suala la ufufuko ni la kweli kabisa na si la uzushi kama wanafalsafa hawa wanavyodai. Anaanza hoja yake kwa kumtaja Yesu-yeye alishuhudiwa na watu tena kati yetu akifa msalabani kabisa, akafa na akazikwa-lakini pia alishuhudiwa na baadhi yetu akiwa amefufuka tena ikiwapo mimi-sasa anawauliza-ninyi mnasemaje kuhusu hili? Ni uzushi tena? Anawaambia jamani bakini katika imani yenu-msidanganywe na hawa watu; mtumaini Kristo.
Ndivyo inavyotokea na kwetu ndugu zangu. Bado tunadanganywa na falsafa mbalimbali na kuziungamia. Tumedanganywa na mitandao mbalimbali na kupotezea muda huko kana kwamba kila kitu kisemwacho nayo ni sahihi. Tunajisikia hofu kubwa pale tunaposafiri bila simu kuliko pale tusafiripo bila hata rozari mfukoni. Tunakuwa tayari kuacha rozari au hata biblia kuliko simu-lengo ni kwamba simu itatulinda, itatuburudisha kwa kutupatia habari mbalimbali za kwenye mitandao. Tuna hofu yakukosa habari kuliko kukosa kanisani.
Kwenye somo la kwanza tunakutana na Yesu akimpinga mfarisayo aliyepinga yeye kupakwa mafuta na mama mmoja. Haya ni matendo aliyoyashindwa yule mfarisayo lakini akayaweza yule mama. Yule mama alionesha heshima kwa Yesu kuliko huyu mfarisayo. Mfarisayo aliona wivu kana kwamba yule mama alikuwa akijipatia sifa zaidi kuliko yeye. Hata majibu yake anayomueleza Yesu chanzo chake ni wivu. Anataka Yesu asitendewe uzuri kwa sababu ya wivu wake. Hata na sisi tupo hivihivi ndugu zangu. Wengi wetu tuna wivu; hatutaki wengine watendewe wema na sisi hatuko tayari kuwatendea. Tukiona wengine wakiutenda tunakasirika, ati tunataka wasifaidi? Tukiona wengine wakitendewa wema yabidi tufurahi zaidi. Kama huwezi kuutenda wema, mwingine ataweza.
Maoni
Ingia utoe maoni