Jumatano, Septemba 09, 2020
Jumatano, September 9, 2020,
Juma la 23 la Mwaka wa Kanisa
1 Kor 7: 25-31;
Zab 44: 11-12, 14-17;
Lk 6: 20-26
KIU YA KUTAKA FURAHA!
Karibuni tena ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu inaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na mtume Paulo akiendelea kukabiliana na matatizo yaliyokuwa yanaikumba jumuiya ya kikristo ya Korintho. Tayari alikwishaanza kulizungumzia suala la uzinzi na uasherati juzi, jana alionya kuhusu kushtakiana kwa watu wasiomjua Kristo na leo basi anazungumzia juu ya mtindo wa maisha ya kuoa na kuolewa.
Anasema kwamba mtu aweza kuishi ukristo wake vyema akiwa ameoa au hajaoa. Kuishi bila kuoa au kuolewa ni jambo jema kwani kwa kitendo cha mkristo kukubali kubakia bila kuoa au kuolewa kwa sababu ya Kristo tayari maisha ya mtu kama huyu ni ushuhuda tosha; amekwishamtangaza Kristo kwamba ni wa muhimu kuliko vyote katika ulimwengu huu. Hivyo Paulo anasema maisha ya namna hii kweli ni bora.
Lakini changamoto ilikuwa hii: wale wasiooa au kuolewa kushindwa kujizuia na tamaa za mwili na hivyo kujikuta wanaanguka kila mara. Hivyo basi wale waliooa au kuolewa waliishia kuonekana kuishi vyema na kuwa bora zaidi na wakitoa ushuhuda juu ya Kristo kwa mapana zaidi kuliko wasiooa au kuolewa. Paulo sasa anasema kwa hali kama hii, basi kila mmoja achunguze tamaa zake na kweli kama huwezi kuzuia tama za mwili, basi afadhali uoe au uolewe na hapa utamshuhudia Kristo kwa mapana zaidi. Lakini changamoto inayobakia ni kila mmoja kupambana na tamaa.
Haimaanishi kwamba ukishaoa tamaa ndio umezimaliza. Hapana, kuna waliooa au kuolewa tayari lakini bado tamaa zao ni kubwa sana, wanatamani na kukwaza zaidi. Hii ni changamoto kwa kila mkristo. Tunatakiwa tuyalete maisha yetu mbele ya Kristo tukimwambia Bwana tufundishe kupambana na hizi tamaa. Tukishaendekeza tamaa, hata mara moja hatutaweza kupambana nazo. Hata ukioa basi utazidi kuziendekeza.
Lakini zaidi ni kwa wale wakristo wasiooa au kuolewa jamani ni kujiepusha na tamaa. Tamaa zinatufanya tusimshuhudie Kristo. Halafu pia epuka mazingira mabaya. Usiyaendekeze kwani yatakufanya ushindwe kuwa shuhuda. Sisi tusiooa tutambue kwamba matendo yetu yanamchafua Kristo mbeleni mwa watu kwa haraka zaidi.
Kwenye somo la injili, Yesu anatoa matumaini makubwa kwa kutoa fundisho juu ya heri. Somo hili ni faraja hasa kwa baadhi yetu basi ambao ndani ya hii dunia tunadharaulika, tusiosoma, sisi mafukara au tunaopigika na kuonwa kuwa si kitu au tunaosengenywa na kusemwa na kila mtu. Tunaelezwa kwamba duniani sio mwisho au kila kitu. Kuna tumaini jingine; waweza kudharaulika hapa lakini jipe moyo, mtumainie Mungu kwani hapa sio mwisho.
Na somo hili ni onyo hasa kwa wale wanaojiona kwamba wamenyookewa na mambo, wanacheka, na kuimiliki dunia na kila kitu kiko safi na kila mmoja anawapenda. Ni onyo kwamba wajichunguze kwani hapa duniani sio mwisho. Sifa za dunia zaweza kukukosesha mbingu. Tupanie ya mbinguni zaidi. Tuchunguze njia zetu na kubadilika zaidi.
Maoni
Ingia utoe maoni