Jumapili, Septemba 06, 2020
Jumapili, Septemba 6, 2020
Dominika ya 23 ya Mwaka
Ez 33: 7-9;
Zab 94: 1-2, 6-9;
Rom 13: 8-10;
Mt 18: 15-20
KUJENGA JUMUIYA YENYE KUWA NA TAHADHARI!
Wakati watu wameshakutana na ugumu fulani, wanakuwa wanatoa kiashirio kwa wengine kwamba muelekeo sio mzuri, viashirio vyao mara nyingi wengi hawa vitilii maanani. Lakini katika hali ya kweli, wengi hupenda kuwatazama wengine wakiwa katika njia isio faa. Mara nyingi wanawachukia, kuwatania na kuwaona wajinga. Mungu analinganisha kazi ya nabii Ezekieli na ya mlinzi. Alikuwa apewe onyo kutoka kwa Mungu naye alipeleke onyo hilo kwa kila mtu. Kazi ya Kanisa na ya kila mkristo ni sawa sawa. Ni kuwaongoza watu kwa ujumbe wa neno la Mungu. Siku hizi tunatumia teknolojia yenye nguvu kuwapa watu ishara ya hatari ya kujisahau kushika neno la Mungu. Tunachofanya leo na teknolojia kilifanyika katika Biblia, ambapo waliwaweka walinzi katika sehemu Fulani ili aweze kutoa ishara ya hatari wakati aduia anataka kukaribia.
"Mtu mmoja alikuwa akishanga shangaa aliokota ufunguo bondeni karibu na mlima mkubwa. Ulikuwa ni ufunguo wa ajabu, ufunguo ambao ulikuwa na uwezo wakufungua kila aina ya nyumba yenye hazina ulimwenguni. Kwa ufunguo huu alikusanya dhahabu na almasi kutoka katika sehemu mbali mbali alizopenda duniani. Akiwa njiani akirudi alisikia sauti ikimwambia kutoka chini ya mlima: “kabla haujatoka nje, hakikisha hausahau kitu muhimu kuliko vyote. Gafla mlango ukafunga moja kwa moja. Alikuwa amesahau kuchukua ufunguo.”
Mwanadamu daima anatafuta kupata ufunguo wa furaha, Amani na kujitosheleza. Sisi wote tunatafuta ufunguo wa urafiki, kueleweka, kuwa na jina na uzuri, na kuwa na kazi nzuri yenye kuvutia na faraja. Wengine wanatafuta furaha kwa fedha, madaraka nk. Lakini hivi vyote vinatufunga na kujikuta tunapotelea huko. Vinatufunga kiasi ambacho tunasahau kitu muhimu ziadi nacho ni ufunguo wa maisha. Maisha ya Ukristo yanatufundisha kwamba dunia hii itapita, hiki ndicho tunacho paswa kuzingatia kwa macho yetu na kutazama “maisha ya umilele”. Hii inamaana kwamba maisha yetu hapa duniani yana lengo zaidi ya lengo la kawaida. Furaha tulio nayo hapa sio kitu, ni kivuli tu cha furaha halisi ambayo tutakuwa nayo huko mbinguni. Lakini ufunguo wa furaha ya maisha haya uko wapi?
Katika somo la Injili ya leo Yesu anatuonesha picha nzuri ya jumuiya ya mapendo na yenye kujali. Inatuonesha ni kwa jinsi ghani tunaweza kuanzisha jumuiya ya kweli ya Kikristo na yenye kupendana.
1. Kama mtu akikukosa, tunapaswa tumwendee kwa upendo wa Kimungu na kumrudisha kundini. Tofauti kabisa na kumlaumu na kuanza kumlaumu, tunapaswa kumfuata kwa mapendo na kumsihi katika mapendo yetu. Injili inatushauri kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja, kwa utulivu na katika hali ya upekee, katika hali ya kurekebishana kindugu, ili kuanzisha tena urafiki uliyo vunjika. Kama hili litashindikana inashauriwa kuchukuwa watu wenye hekima na kumfuata kumuonesha kwamba jumuiya nzima inakuhitaji kurudi kundini katika mapendo yote.
2. Yesu anasisitiza nguvu ya sala. Anasema “pale wawili au watatu walipokusanyika kwa ajili yangu, Baba atakuwa katikati yao”. Huu ni uhakika anaotoa Yesu kwamba wale wanaosali yeye atakuja katikati yao na kuwa kati yao na kushiriki katika sala yao. Wayahudi walikuwa na Imani kubwa katika sala za pamoja. Iliandikwa “wawili walipo kusanyika na wanajihusisha na kujifunza Torati, utukufu wa Mungu upo katikati yao” sala za jumuiya huweka magomvi mbali na kuleta umoja. Agano, jumuiya, ukarimu, msamaha hizi ni sifa za dini ya Kibiblia. Uzoefu wa haya yote vinafanya maisha yetu kuwa na furaha, na kuishi vizuri. Haya yote yanawezekana tu pale ambapo tuna upendo. Kwa mfano,
"Mfungwa mmoja alikuwa anarudi nyumbani, kutoka katika mahabusu ya mbali akiwa kwenye treni. Alikuwa akiona aibu kwa kufungwa kwake na alikuwa akidhani familia yake itakuwa imemsamehe. Kwa ishara ya kuonesha kwamba wamemsamehe, walipaswa wafunge riboni nyeupe kwenye mti ambao ulikuwa karibu na gari nyumbani kwake. Hivyo kama hataona riboni nyeupe kwenye mti, yeye atapitiliza na treni aelekee kokote atakapo kwenda. Wakati treni ilivyofika karibu na nyumbani, akawa na wasi wasi mkubwa kiasi ambacho hakuthubutu kutazama kupitia dirishani. Marafiki zake wakaamua kubadilisha nafasi wakisema tunafahamu tu ataangalia mti uliokaribu na gari. Ghafla akanyanyua kichwa bila kujua na tazama sio roboni moja iliyowekwa kwenye mti bali mti wote ulikuwa umejaa riboni"
Amani na mshikamano unawezekana tu, pale ambapo watu wanaishi kwa roho ya upendo na msamaha. Mungu ni upendo na penye upendo Mungu yupo. Upendo wa Mungu unabeba pia upendo kwa jirani. Upendo tunaweza kuupata tu tunapo amua kuishi na wenzetu, kwa mshikamano katika jumuiya. Hili halimuumizi mtu yeyote, bali linakamilisha kila kitu na kufanya maisha yafikie katika kilele cha hali ya juu.
Mungu ametufanya sisi tuwe walinzi wa dunia sasa. Tunapaswa kuwa walinzi, kutangaza kwa kila mmoja, jumuiya zetu, na ulimwengu wa ukweli katika Yesu Kristo. Tunaitwa kusimama pamoja, bila kuachana katika Imani bila kuogopa kuitwa tusio na maana au mafundisho potofu, bali tutangaze kwa jirani na jumuiya zetu, ili watu wafahamu katika kutokufahamu kwao, kumuamini Yesu, na kukuwa katika neema na utakatifu. Tunapaswa kuwasaidia wengine watambue makosa yao, hasa tukiwa na kazi kama ya wazazi kwa mtoto, mwalimu kwa wanafunzi, wazee na vijana.
Tutumie njia sawa ya kuwasaidia wengine watoke katika makosa yao bila ya kuwaumiza au kuwadhalilisha na kuwaachia makovu. Badala ya kuponya tukakuza kidonda zaidi. Katika vikao vyetu tuangalie njia njema ya kumsadia mtu na kumuonya badala ya kumwanika hadharani mbele ya watu wote, kama kuna njia nzuri ya mtu mmoja kumfuata kwa hekima utamsaidia zaidi, kuliko kumkosoa mtu mbele ya watu wengi au katika kikao, hili haliponyi kwani mmoja hujisikia amedhalilishwa na utu wake kudharauliwa. Mfano tusisubiri mpaka mtu afe ndio tupate muda wa kukaa pamoja tuje kumrekebisha mtu mbele ya kikao cha ukoo, badala yake tutumie njia mbadala ya kutuma mtu mwenye hekima amsaidie na kupatana kabla ya kukaa pamoja. Kutangaza dhambi ya mtu mbele ya kikao, daima haina lengo la kuleta upatanisho wa kweli badala yake humuachia mtu maumivu na kisasi moyoni. Hakuna hata mmoja wetu angependa dhambi yake itajwe mbele ya watu. Ndio maana sakramenti ya kitubio husaidia kweli. Tumuige Yesu aliyekuwa na huruma kwa wadhambi.
Sala:
Bwana, upo nasi katika jumuiya yetu, tukishikana pamoja kwa mapendo, huruma na msamaha. Tunakuomba tuwe watu wakutafuta furaha, upendo na Amani. Tunakuomba tuwe tayari kusamehe na kupatana na kila mtu. Yesu, ninakuamini wewe.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni