Jumanne, Septemba 08, 2020
Jumanne , Septemba 8, 2020,
Juma la 22 la Mwaka
Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Bikira Maria
Mik 5: 1-4 au Rum 8: 28-30;
Zab 12: 6;
Mt 1: 1-16, 18-23
MUNGU ANA MPANGO NASI!
Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo basi ni siku ya furaha kwani kanisa linaadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Bikira Maria Mama wa Mungu. Sherehe hii chanzo chake ni baada ya ule mtatguso wa Efeso wa mwaka 431 uliomtangaza Maria kama Mama wa Mungu na kukataa uzushi wa Nestorius.
Nestorius alidai kwamba yule aliyezaliwa na Bikira Maria hakuwa Mungu bali alikuwa mwanadamu mkombozi. Hivyo alikataa kumtambua Bikira Maria kama Mama wa Mungu. Baada basi ya huu mtaguso, kuukataa uzushi huu, kulitokea ibada nyingi za kumumheshimu Bikira Maria nafasi yake katika ukombozi. Sherehe ya kuzaliwa Bikira Maria iliwekwa kutokana na nafasi yake katika historia ya ukombozi-yaani kwa sababu yeye ndiye aliyemzaa Kristo, siku yake ya kuzaliwa ilipoonekana tu, basi dunia iliingia kwenye matumaini mengine, ilipata ahueni na mwanzo mpya kama kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji kulivyokuwa- ni baraka kwa dunia, chanzo cha furaha, siku ya ukombozi ukiimarika na matumaini kujaa.
Ndivyo ilivyotokea kwa Bikira Maria ndugu zangu!
Na kanisa huadhimisha sherehe za kuzaliwa za watu wawili tu-Yohane na Bikira Maria kutokana na nafasi yao katika historia ya wokovu.
Ndugu zangu, kuzaliwa kwa Bikira Maria kulikuwa neema kwa dunia na kweli aliitendea dunia mengi. Nasi basi tukumbuke kwamba kuzaliwa kwa kila mmoja ni zawadi Mungu anayoipa ulimwengu ili izalishe na kutenda mema kwa ajili Mungu na ulimwengu. Tutambue hili ndugu zangu.
Tujiulize, je, pale ninapoishi kweli mimi ni zawadi? Je, ninaleta matumaini kwa hili eneo? Ni wangapi nimewatesa vya kutosha au kuwaibia? Ni wangapi waliokuja kuchukua ulinzi na msaada chini ya mabawa yangu. Pengine wengi wetu ni wafisadi na waongo na wachonganishi na wambea na tabia hizi zinanifanya nisiwe neema kwa ulimwengu. Lazima niwe baraka, zawadi kwa ulimwengu kama Maria.
Kingine ni kujua kwamba kama kila mtu ni zawadi, basi tuachane na uuaji wa vichanga hasa utoaji mimba. Kila mmoja ni zawadi.
Kwenye somo la injli tunakutana na Bikira Maria akipata habari za kumzaa mkombozi Yesu Kristo na kweli alimzaa na kuiletea dunia nafuu. Na kweli alijitunza sana hadi akaweza kumzaa huyu mkombozi vyema. Wengi kati yetu hatujitunzi, tunajichafua na kweli Mungu ameshindwa kututumia kwa ajili ya kuuletea ulimwengu matumaini. Karama mbalimbali tumezinyanganywa kutokana na majivuno, hivyo tumeshindwa kuwa matumaini kwa wenzetu. Tujitunze na kujipalilia na tutakuwa na mengi ya kuzaa. Tuache majivuno.
Maoni
Ingia utoe maoni