Jumamosi, Septemba 05, 2020
Jumamosi, Septemba 5, 2020.
Jumamosi kumbukumbu ya Bikira Maria
Kol 4: 6-15
Lk 6: 1-5
KUONDOKANA NA MZIGO WA MTAZAMO MBAYA!
Sabato ilikuwepo hata kabla Torati haijatolewa katika Mlima Sinai (Kut 19). Wayahudi walifundishwa “kukumbuka siku ya Sabato” na kuifanya takatifu. Siku ya sabato ilitegemewa kuwa siku ya mapumziko na siku ya kuabudu, muda wa kukumbuka siku aliyo pumzika Mungu baada ya kazi ya uumbaji, siku ya saba. Mafarisayo walichukulia kitendo walichofanya wafuasi kwenye Injili kuwa ni kufuru kuhusu Sabato. Walivyo mlaumu Yesu kuwa ameikufuru Sabato, Yesu aliwajibu vyema. Yesu alimtumia Daudi kama mfano, wakati Daudi akimkimbia Sauli alikula mikate ile ya Wonyesho (iliobarikiwa) inayotumika tu pale Mahali Patakatifu (tabernacle) ambayo ililiwa na makuhani pekee. (Sam 21: 1-6). Yesu anasema wazi kwamba Sabato sio Bwana, bali Mwana wa mtu (Yesu mwenyewe) ndiye. Ni yeye mwenyewe mwenye mamlaka ya kubadili torati na sheria ya Sabato.
Yesu anatufundisha tusifungwe mno na sheria tushindwe kuonesha upendo kwa jirani zetu. Pamoja na kutimiza majukumu yetu, tusisahau kwamba sisi tunayo sheria ya Kristo ambayo ni upendo, sheria isiyo na upendo si sheria ya Kristo. Tafakari leo juu ya juhudi zako juu ya kuwa na mtazamo mbaya kwa wengine. Kama unafanya hivyo basi tambua Mungu anapenda ubadilike na akutoe katika mzigo huu. Tusitumie sheria za Mungu kuwatishia watu na kusahau, Yesu alivyokuwa na huruma kwa wadhambi, na watu wote.
Sala:
Bwana, naomba nikuheshimu katika kazi yangu na katika mapumziko yangu na niwatendee jirani zangu kwa heshima na upendo. Niweke mbali na roho ya mabishano na ubinafsi ili niweze kutafuta uzuri wa jirani zangu katika hali zote. Yesu nakuamini wewe.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni