Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Septemba 04, 2020

Ijumaa, Septemba 4, 2020,
Juma la 22 la Mwaka wa Kanisa

1Kor 4: 1-5;
Zab 36: 3-6, 27-28, 39-40;
Lk 5: 33-39

HAKUNA KIRAKA; HAKUNA KUCHANGANYA!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Somo la kwanza Paulo anazidi kujibu hoja za baadhi ya wakristo waliokuwa wakimkejeli yeye kama mhubiri kwamba hakuwa na ubora au kiwango; alikuwa na kiwango cha chini kuliko akina Apolo. Paulo anasema kwamba waachane na kumshabikia mhubiri kana kwamba ni Mungu; wahubiri ni vyombo tu vinavyotumiwa ili vipeleke au kubeba siri za Mungu. Hivyo mhubiri yeyote ni lazima awe mwaminifu, na ajitahidi ili basi mwishowe aweze kukutwa akiwa imara kwa imani yake na mwaminifu kwa kile anachokihubiri.

Hili ndilo litakalokuwa jambo la mafanikio makubwa kwake. Na anasisitiza kwamba wasidhanie ati ni kwa kufikiriwa na kuonekana wazuri mbele ya macho ya wanadamu ndio basi wanavyoweza kujiona kwamba wao ni thabiti; hapana, wasivimbishwe vichwa kabisa na hizi sifa za wanadamu. Hizi hazifai kitu kabisa kabisa. Bado wa kuwafanyia majaribio sio wao bali ni Mungu mwenyewe na bado ni hadi ile siku ya mwisho; hapa Mungu mwenyewe atatoa hukumu.

Paulo anasema hivyo kwa sababu yeye mwenyewe alishashuhudia kwamba wahubiri wengi hasa wale maarufu hawadumu hadi mwisho. Huishia kuwa wazushi na kuwaangusha waamini. Hivyo anawaambia waamini kwamba mambo bado. Mtu unatangazwa mtakatifu ile siku ya mwisho.

Ndugu zangu hapa tunalokubwa la kujifunza; ni kweli kwamba kuna kitendo cha baadhi yetu kushabikia wahubiri au waalimu, tunasema mhubiri huyu ni bora sana, anafika mahali anachukuliwa kama Mungu, na nafasi ya Yesu inachukuliwa hata na mhubiri huyu. Na mhubiri akisikia hivyo anajivuna na kichwa kuvimba na hata kushindwa kuiona nafasi ya Yesu maishani mwake. Na huku tayari kumekwisha waangusha wahubiri wengi sana. Hii sio sahii, wahubiri tusiridhike kwa kushabikiwa shabikiwa na sisi wenyewe tuache kushabikia wahubiri. Ni Yesu tu ndiye wa kushabikiwa. Mhubiri ni chombo tu.

Kwenye injili Yesu anasisitiza kwamba divai mpya iwekwe kwenye viriba vipya kwani ikiwa itawekwa kwenye vya zamani, basi itavipasua vile vya zamani na divai yote kumwagika. Hapa viriba vinamaanisha moyo wa mkristo unaopaswa kuwa mpya ili basi uweze kumpokea Kristo. Wayahudi leo kwenye injil wanataka Yesu aendelee na tamaduni na desturi zilezile za zamani hata baada ya ujio wake kama Masiha. Yesu anawaaambia kwamba hizi ni zama mpya.
Tunahitaji viriba vipya.

Baadhi ya Wayahudi walikwenda na viriba vya zamani na mioyo yao ikapasuliwa, havikuweza kubeba divai mpya yaani Yesu mwenyewe. Sisi lazima mioyo yetu tuiandae kwa kuungama, tuache ya kizamani kama ushirikina, tumpokee Kristo. Wengi mioyo yetu imekwishapasuliwa tayari, viriba vyetu vimekwishapasuka kwa sababu tunakwenda na ya kizamani mbele ya Yesu. Kristo hachanganywi na ya zamani. Tuache chuki na aina yeyote ya masengenyo. Tumpokee Yesu

Maoni


Ingia utoe maoni