Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Septemba 02, 2020

Jumatano, Septemba 2, 2020,
Juma la 22 la Mwaka wa Kanisa

1 Kor 3: 1-9
Zab 32: 12-15, 20-21
Lk 4: 38-44

NGUVU YA MAMLAKA!

Karibuni ndugu zangu kwa kwa adhimisho la Misa Takatifu. Tafakari ya neno la Mungu leo basi katika somo la kwanza tunakutana na mtume Paulo akiendelea kujibu tuhuma zilizo elekezwa kwake kwamba kwa nini hakuhubiri kwa kutumia falsafa au ujuzi fulani wa lugha kama labda walivyofanya wahubiri wa dini mbalimbali au hata kama alivyofanya mhubiri mwenzake kama Apolo ambaye alikuwa msomi na mwanafalsafa bora kabisa.

Paulo anawambia kwamba aliamua kutumia lugha rahisi na mtindo mraisi kwa sababu wao wenyewe waliuhitaji mfumo huo kwani bado walikuwa ni wachanga kiimani. Wachanga kiimani walishwe kile wanachoweza kuelewa kwa ufasaha mzuri zaidi. Hii ndiyo iliyokuwa nia ya Paulo. Lakini wengi kati ya waamini walishindwa kuona hii nia njema toka kwa Paulo , wakamuona kuwa ni dhaifu na mwenye uwezo mdogo na kutaka wahubiri machachari wenye kujua falsafa. Hivyo basi wakaishia kugawanyika, wengine wakajiita sisi ni wakristo lakini mhubiri wetu sio Paul, ni Apolo, wengine ni wa Kefa-lakini yote haya yalikuwa ni majivuno tu.

Suala hili linafanana na malalamiko ya kila siku ya baadhi ya wakristo-kwamba ati hatuna wahubiri wazuri, hatulishwi inavyostahili, oo tunalala kanisani, huyu mhubiri hajui kuchangamsha, siku tukichekeshwa ndio tunafurahi, tukija kanisani tunataka wahubiri wanaoruka, na kupiga kelele-jamani, lazima kuchunguza suala hili-tujiulize kwanza-je, kweli hili ni jambo la kweli au ni kwa sababu ya tamaa zetu zinazonifanya niongee namna hii-kweli simkosei haki yule mhubiri ninayemlalamikia?

Nataka awe anachekeshachekesha watu? Kanisani sio sehemu ya kufanyia usanii au comedy-lazima kutambua kwamba mhubiri yeyote akilitumia kanisa kama sehemu ya kufanyia mambo kama haya, anakosea sana. Hivyo tuache hizi tamaa zetu za kutamani wahubiri ati wenye kuchangamsha. Kristo ndiye wa kukuchangamsha na sio mhubiri. Basi haya mawazo ni vizuri kuyaacha.

Katika injili yetu, tunakutana na Yesu akiwa faraja kwa watu, akiwaponya wagonjwa wao, na watu kufikia hatua ya kufurahi kupita kiasi cha kutaka abakie huko kwao lakini Yesu anakataa na kusema kwamba yeye lazima aende sehemu nyingine kwani wanahitaji nako na neno la Mungu. Hili ndilo linalokosekana kati ya wahubiri wengi wa leo.

Wengi tunatafuta kumiliki wafuasi, tunawataka wawe wetu, na hata hatutaki kuhamia sehemu nyingine tukifikiri kwamba ati tukiwakosa wale wafuasi, basi mambo kwisha. Hili sio sawa ndugu zangu. Kristo ndiye tunayepaswa kummiliki na sio hawa wafuasi. Mhubiri na mfuasi ni mali ya Mungu. Kuwa mali ya Mungu nawe utabarikiwa zaidi na acha kuwa mali ya mhubiri au kutaka kumiliki wahubiri kama wanavyoonywa wakristo wa leo toka Korintho.

Maoni


Ingia utoe maoni