Alhamisi, Septemba 03, 2020
Alhamisi, Septemba , 3 2020,
Juma la 22 la Mwaka wa Kanisa
KumbuKumbu ya Mt. Greogori Mkuu , Papa na Mwalimu wa Kanisa
1Kor 3: 18-23;
Zab 23: 1-6;
Lk 5: 1-11
KATIKA KUVUA SAMAKI NA KUVUA WATU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Paulo bado kwenye somo la kwanza anazidi kujibu hoja za baadhi ya Wakorintho waliomkejeli kwamba yeye basi hakuwa mtaalamu au na ufundi wa uhubiri bora; yaani hakuelezea mambo katika lugha nzuri sana na hivyo kushindwa kuwavutia waamini kama walivyoweza kwa wahubiri wenzake hasa akina Apolo ambao walizijua falsafa za Kigiriki na walihubiri kwa kutumia ujuzi toka kwenye falsafa hizi.
Paulo anajibu na kusema kwamba wasidhanie kwamba kile kinachosifiwa duniani na mbinguni ni hivyohivyo, au vile vionjo vinavyopendwa na dunia wasifikiri kwamba na mbinguni vitakuwa vinapendeka. Anawahabarisha kwamba watambue kwamba kile dunia inachoweza kukiona kama hekima kuu kabisa, mbele ya Mungu waweza kukuta ni ujinga mtupu; kwani mawazo ya Mungu sio mawazo ya mwanadamu. Anatoa angalisho kwamba sio kila kinachosifiwa na dunia basi kichukuliwe kama hakina kosa.
Somo hili latufundisha somo kali hasa kwa maisha yetu. Ni kweli baadhi ya sifa za kidunia zinatudumaza kiroho, zinaweza kutudumaza kiroho sana kwani pale panapohitaji ujishushe na kuomba msamaha, dunia inaweza kukuambia kwamba hapa hakuna haja ya kuomba msamaha huo, dunia inasifia mawazo ya kibabe, unakuta wasanii au wale wahubiri wanaoruka juu huku na huku bila hata kuongea kitu ndio wanaoonekana kuwa wanahubiri vizuri, wengine wakaonekana kwamba wako hewa na kusababisha waamini walale kanisani. Kumbe ukichunguza-sababu hii sio kweli, ni uvivu wetu. Sasa wewe mhubiri ukivimbishwa kichwa na sifa hizi basi unaishia kupotoka tu, hufiki mahali.
Kwenye somo la injili tunakutana na habari kwamba akina Simon Petro walikuwa wamekaa muda mrefu, usiku mzima bila kuvua chochote. Lakini basi baada ya kufuata maagizo toka kwa Yesu, waliweza kuvua samaki wa kutosha. Hili ni fundisho kwetu ndugu zangu. Kuna wakati kweli tunakazana kama hawa wanafunzi, tunatumia nguvu zetu, tunamwaga pesa nyingi tukikazana kufanya kitu-lakini akisogei popote. Hata kama ni kazi ya shule-waweza kumaliza masaa ukikazana lakini ukashindwa kuandika hata mistari mitano. Lakini basi ukija mbele ya Mungu, ukijikabidhi kwake unashangaa ile kazi unamaliza ndani ya muda mfupi. Huu ni mwaliko kwetu kwamba tupende kujikabidhi mikononi mwa Mungu kabla ya kufanya chochote. Tunapoteza muda mwingi mno tukikazana kufanya vitu wenyewe. Akiwako Yesu, hakika tutafaulu vizuri na mapema zaidi.
Pia Yesu anatupatia jambo la hadhi zaidi. Anatufundisha kuwa wavuvi wa watu na kuachana na uvuvi wa visamaki. Wengi wetu tunapoteza muda kuvua vitu visivyokuwa na hadhi, katika ulevi, umbea, uasherati na hivi havitufikishi popote. Yesu atatupatia muongozo wa kutamani makubwa zaidi.
Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni