Jumanne, Septemba 01, 2020
Jumanne, Septemba,1, 2020,
Juma la 22 la mwaka wa Kanisa
1 Kor 2: 10-16
Zab 144: 8-14
Lk 4: 31-37
VITA VYA KIROHO!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Bado tunaendelea kuongozwa na tafakari ya somo la kwanza toka katika barua ya kwanza ya Mtume Paulo kwa Wakorintho ambapo basi tunakutana na mtume Paulo akizidi kujitetea dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwake kwamba alifundisha kwa namna ambayo haikuambatana na falsafa za kiulimwengu na mafundisho yake hayakutumia mfumo wa falsafa hizi ambazo kwa kipindi hicho, zilionekana kwamba ndizo zenye uwezo mkuu zaidi ya elimu yoyote.
Paulo leo anasema kwamba ili uweze kuyatambua yamhusuyo Mungu, unahitaji Roho ya kimungu ambayo asili yake si ulimwenguni. Ansema kwamba wengi tunakosea kwa sababu ya kufikiri kwamba roho ya kidunia inauwezo wa kufahamu na kutoa maelezo juu ya kila kitu. Hapa ndipo wengi tumekosea. Hili fundisho latufaa sisi hasa kwa nyakati zetu ndugu zangu ambapo baadhi yetu hasa wale tuliobahatika kusoma kidogo tunaishia kuukataa uwepo wa Mungu au kutokufuata maongozi ya viongozi wetu wa dini tukifikiri kwamba tunajua kila kitu. Tutambue kwamba kamwe hatuna uwezo wa kuweza kuyafahamu yamhusuyo Mungu bila ya yeye kuamua kutufunulia. Na yeyote aweza kufunuliwa; sio tu yule aliye na elimu! Hivyo tubakie wapole siku zote mbele ya Mungu.
Hata kwenye kuchangia neno la Mungu tuwapo katika jumuiya zetu, tumpatie kila mmoja nafasi-na kusikilizwa. Hata yule asiye na kisomo cha kutosha aweza kulichambua neno hilo ikiwa Bwana atamvuvia Roho wake.
Katika somo la Injili, tunagundua kwamba pepo mchafu anaanza kwa kumsifia Yesu, kumkiri kama mtakatifu wa Mungu, na kujionesha kwamba hata yeye kama pepo anaukiri utakatifu huu na ukuu wa Yesu. Lakini lengo lilikuwa ni ili Yesu amwonee huruma pepo kumwacha aendelee na kazi ya kuwatesa watu. Lakini Yesu anatambua kwamba pepo ni kiumbe mchafu siku zote na si wa kufanya urafiki naye.
Nasi ndugu zangu tuepuke kufanya urafiki na pepo-wale waliowabaya lakini wanatusifiasifia tu ili tuwaache na kuwahurumia-wale unaokuta kwamba ni wezi kitengo chako lakini anakusifiasifia tu ili basi umwache. Hawa ni pepo na tusianzishe urafiki nao. Mwishowe watatuangusha kabisa. Watu wa namna hii au tabia za namna hii tuzikemee mara moja kama Yesu alivyomkemea yule pepo mbaya na kumwacha asije akamwangusha baadaye. Wengi wameangushwa kwa kupewa sifa za namna hii na kuvimba kichwa wakaishia kupoteza yote. Sisi tusikubali sifa za uongo namna hii.
Maoni
Ingia utoe maoni