Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Agosti 31, 2020

Jumatatu, Agosti 31, 2020.
Juma la 22 la Mwaka


1 Kor 2: 10-16;
Zab 119:97-102
Lk 4:16-30

KRISTO ANAONGEA NASI KWA NJIA YA FAMILIA NA MARAFIKI ZETU!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Mungu linaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na mtume Paulo akiendelea kujibu hoja dhidi yake juu ya mahubiri yake kutokutumia falsafa kali na ya kutisha katika kuelezea mafundisho yake ya Kikrosto kule Korintho zaidi kama walivyofanya hata baadhi ya wahubiri wa Kikirsto kama vile akina Appolo.

Korintho ulikuwa mji wa kibiashara na uliojaa wasomi na wanafalsafa wa Kigiriki. Yeye anajitetea na kusema kwamba yeye katika mahubiri yake, alimhubiri Kristo, bila kutumia falsafa au ujanja fulani wa lugha ili kwamba basi nguvu yake Kristo na injili yake ipate kuonekana. Kristo ndiye hekima, ndiye falsafa ya hali ya juu na hivyo basi haihitaji asaidiwe na falsafa za kidunia.

Falsafa za kidunia zingalitumika zaidi, mwishowe nguvu ya injili ya Kristo ingalishindwa kuonekana. Paulo anazungumza hivi kuwafanya watu wajue maana ya Imani; baadhi ya Wagiriki walifikiri kwamba mtu mwenye elimu ya falsafa anaitambua Imani zaidi na yeye ndiye mwenye ujuzi wa kiimani na ni bora kuliko asiye na elimu. Lakini Paulo anaonesha kwamba cha kwanza ni Kristo, sio falsafa, Kristo ndiye ambadilishaye mtu, awezaye kumwokoa mtu na si falsafa. Hivyo basi ni lazima uwezo wake usisitizwe kwa upekee kabisa.

Ndivyo ilivyo ndugu zangu. Kumtambua Kristo na kuiona nguvu yake aihitaji tuwe wasomi sana. Iliyopo ni ule uwezo wa kumpokea kama Bwana na Masiha. Huu ndio ulio wa muhimu. Hivyo tuwaheshimu wote mbele ya Kristo. Na hasa sisi tuliobahatika kuwa na elimu ya kidunia, tujitahidi zaidi. Nguvu ya injili ya Kristo yaweza kudhihirika hata kwa asiye na elimu kubwa ya kidunia. Sisi tuliobahatika kupata elimu ya kidunia, tuwe wanyenyekevu tuwapo mbele ya Kristo, unyenyekevu utatusaidia tuione nguvu ya Kristo maishani mwetu.

Ni jambo la kusikitisha kama sisi ambao ni waalimu, maenginia, na madaktari-tunafahamu mengi kuhusu elimu dunia lakini basi tukashindwa kufahamu juu ya nguvu ya Kristo na injili yake. Tuwe wapole mbele ya Kristo na hakika tutaiona nguvu hii. Elimu yetu isitutie kiburi; tuwe wapole na kweli tutaweza kuiona nguvu ya Kristo maishani mwetu.

Kwenye somo la Injili, watu wa nyumbani mwa Yesu walishindwa kuwa wapole na wanyenyekevu mbele ya Yesu na hivyo basi wakashindwa kumfaidi Yesu kama walivyofaidi watu wa maeneo mengine. Walishindwa kujishusha mbele yake, Walijiona kuwa wajuaji kumshinda Yesu, walikuwa ni wagonjwa wakashindwa kujitambua.

Sisi tuwe wanyenyekevu mbele ya Yesu. Haijalishi umesoma hadi wapi, una pesa kiasi gani au cheo gani-uwapo mbele ya Yesu, ni lazima tuanguke magoti mwake na hili litatuwezesha kuiona nguvu yake maishani mwetu. Tusitiwe kichwa na elimu au chochote kile. Wengi wetu tumishindwa kumpokea Kristo kutokana na kiburi chetu au mali zetu. Tuache hili.
Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni