Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Agosti 27, 2020

Alhamisi, Agosti 27, 2020,
Juma la 21 la Mwaka


1Kor 1:1-9;
Zab 144:2-7;
Mt 24:42-51


KUWA TAYARI !

Karibuni ndugu zangu kwenye adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Neno la Mungu leo katika injili linasisitizia juu ya kuwa tayari kwani hatujui siku wala saa. Anatoa mfano kwamba suala la kukesha tunalifanya kwenye maisha yetu ya kila siku wakati tunalinda vitu vingine kama gari lako au simu yako au tv au nyumba yako lakini basi tunapoambiwa tukeshe tunaambiwa tutende matendo mema muda wote ila ni wachache wanaojua hili au kulifanya.

Mwenye nyumba akisikia kuna mwizi hatalala watawawinda tu hata ikiwezekana kuanza sungusungu lakini wakiambiwa kuna Bwana anakuja hatujali. Hapa Yesu anasisitizia kwamba mwito wa mwanadamu tena mkristo ni kukesha ukitenda matendo mema tukimsubiri Bwana wetu atakayekuja kutuchukua na kutupeleka pale alipo. Hivyo lazima tuwe tunakesha tukimsubiri huyu Bwana.

Wengi kati yetu kwa sababu Bwana huyu ati hatujawahi kumwona kwa macho, tunajiona kwamba hahusiki nasi, hatuna haja ya kukesha kwa mtu ambaye hata hatujawahi kumwona. Lakini tukumbue kwamba japokuwa hatukumkuta kipindi kile akiishi duniani ili basi atupatie hiyo ahadi yake, sisi tunafurahia matunda ya kazi aliyoitendea ulimwengu, wema wake kwa ulimwengu na hivyo basi ni lazima tukeshe tukimsubiri na tunahusika naye sana.

Tutumie kile alichotuachia vizuri-rasilimali zote tulizonazo hapa ulimwenguni ni zake-zitumiwe kwanye kukuza ufalme wake. Tusizitumie ati kwenye kuendekeza uasherati, ulevi, dhuluma au uonevu wowote ule. Jua kwamba ni Mungu kakukopesha tu, huna chako. Zitumie kwenye kukuza ufalme wake na si kwenye kutumia rasilimali za Mungu kwenye kumsaidia shetani akuze ufalme wake. Hapa ndipo kukesha. Kutumia rasilimali zake kama mwazimaji tu na kuukuza ufalme wake.

Wengi tumetumia rasilimali hizi kwenye kumsaidia shetani akuze utawala. Kutumia pesa katika ulevi wa kupindukia na uasherati zote hizi ni kuutumia wema wa Bwana vibaya, ni kutumia zile mali basi kuwatesa wale watumishi wa Bwana na basi ajapo atatuadhibu.

Kwenye somo la kwanza, Paulo anamshukuru Mungu kwa baraka walizojaliwa Wakarintho na jinsi walivyoipokea Injili na kujaliwa vipaji vingi vya kiroho. Hivyo wanapaswa kutumia vipaji hivi kama wakili mwaminifu wa Bwana kwa ajili ya kulijenga kanisa la Bwana. Kila mmoja ajione kana kwamba ameazimwa kitu na Yesu na hivyo basi akitumie kama wakili mwema. Tuache kutumia vipaji hivi kuwasumanga wengine, hapa tutakuwa hatukeshi na Bwana akija, atatuadhibu na kuchukua vipaji vyake toka kwetu. Tumsifu Yesu Kristo

Maoni


Ingia utoe maoni